TSHS.BILIONI 374.5 ZATOLEWA KWA AJILI YA MIKOPO YA NYUMBA NCHINI




Na Jonas Kamaleki, MAELEZO

Shilingi bilioni 374.5 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya nyumba hapa nchini ili kuwawezesha wanachi kuwa na makazi bora ambayo ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani.

“Ili kukidhi mahitaji ya nyumba yanayotokana na ongezeko kubwa la watu, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeshiriki katika utoaji wa mikopo ya nyumba ambapo soko la mitaji na mikopo ya nyumba nchini limeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kwa mwaka jana,”alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, taarifa za Benki Kuu zinaonyesha kuwa idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba zimeongezeka kutoka tano kwa mwaka 2010 hadi kufikia 26 Desemba 2015.

Aidha. Lukuvi amesema kuwa utoaji wa mikopo ya muda mrefu ya nyumba umewezesha sekta binafsi na waendelezaji milki kuingia katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba za biashara na makazi kwa kuwauzia wananchi kwa mkopo wa muda mrefu.

Aliongeza kuwa ili kuwezesha sekta ya nyumba kuendelea kufanya vizuri, Serikali inafanya mapitio ya sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya nyumba, zikiwemo Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000. Lengo la mapitio hayo ni kuweka mfumo wezeshi ambao utarahisisha uendelezaji wa sekta hiyo.

Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) imesaidia kukuza tekinolojia asilia ya vifaa vya ujenzi, kuhamasisha na kusambaza matokeo ya utafiti na utaalam wa ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu, alisema Lukuvi.

Lukuvi amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha ulioisha, Wakala ulitengeneza mashine 80 za kufyatulia tofali za kufungamana ambapo kati ya hizo, mashine 46 ziliuzwa kwa vikundi 12 vya ujenzi. Wakala pia ulitoa mafunzo ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa vikundi 110 katika wilaya za Kahama, Morogoro na Kinondoni.

Waziri Lukuvi amesema kuwa Shirika la Nyumba limeendela kutekelza miradi yake 64 yenye jumla ya nyumba 4,990. Miradi hii imeliwezesha Shirika kufikia mikoa 24 kwa kujenga nyumba za makazi ya gharama nafuu 1,841, gharama ya kati 2,823 na nyumba za biashara 326.

“Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na Mamlaka za Upangaji Miji katika uandaaji wa Mipango Kabambe ya miji, Manispaa na Majiji, hadi kufikia Septemba 30, 2016 Rasimu za Mipango hiyo kwa Jiji la Mwanza, Manispaa za Mtwara, Iringa,Tabora, na Musoma pamoja na Mji wa Kibaha zilikuwa zimekamilika na kutangazwa kwenye gazeti la Habari Leo ili kuwawezesha wadau wa maendeleo kupitia rasimu na kutoa maoni yao,”alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema pia kuwa zoezi la urasimishaji makazi katika jiji la Dar es Salaam unaendelea katika maeneo ya Kimara, Chasimba na Makongo Juu. Hadi kufikia Septemba 2016 viwanja 4,818 vilitambuliwa ambapo kati ya hivyo. Viwanja 4,665 vimepimwa na maandalizi ya umilikishaji yanaendelea.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa Jumatatu ya kwanza ya Oktoba kila mwaka ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na 40/202 lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba 1985. Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yana kaulimbiu isemayo Nyumba Kitovu cha Miji (Housing at the Centre).

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post