WANANCHI WABOMOLEWA NYUMBA 150 JIJINI DAR ES SALAAM, LEO KUTUA KWA MKUU WA WILAYA KUPELEKA KILIO CHAO

 Mkazi wa eneo hilo, Lukia Khalid (aliye kaa), akiwa amekaa nje na vyombo vyake baada ya kubolewa nyumba yake.
 Wananchi wa Tegeta A Kata ya Goba wakiwa wamesimama chini ya mti Dar es Salaam jana, baada ya nyumba zao kubomolewa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa madai ya kuvamia eneo hilo. Hata hivyo wamekanusha kuvamia eneo hilo. Zaidi ya nyumba 150 zilibomolewa. Wananchi hao leo wanaandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kupeleka malalamiko yao.
 Askari polisi wakiwa eneo hilo kuimarisha ulinzi.
 Watoto wakiangalia nyumba yao baada ya kubomolewa.
 Mkazi wa eneo hilo akiwa kando ya nyumba yake iliyobomolewa.
 Mkazi wa eneo hilo akiangalia nyumba yake baada ya kubomolewa.
Magodoro yakiwa yamefunikwa na paa la nyumba baada ya kubomolewa kwa nyumba hizo.

Na Dotto Mwaibale

KAMPUNI ya Udali ya Yono Aution Mart imebomoa nyumba zaidi ya 150 za wakazi wa Tegeta A Kata ya Goba jijini Dar es Salaam kwa madai ya kujengwa eneo ambalo sio lao huku Kaya zaidi ya 450 zikikosa makazi ya kuishi.

Hata hivyo ubomojai huo umepingwa na wananchi hao wakidai eneo hilo ni lao na wapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Zoezi la ubomoaji wa nyumba hizo lililofanyika Dar es Salaam jana, ulisimamiwa na askari polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi huku wakiwa katika magari yenye namba PT, 3475, 1986 na  3675 huko kukiwa na askari hao zaidi ya 15.

Mmoja wa wananchi hao, Macarios Turuka  akizungumza na Jambo Leo eneo la tukio alisema eneo hilo kwa kipindi kirefu lilikuwa halitumiki na lilikuwa ni vichaka vya wahalifu kwani wanawake walikuwa wakibakwa na kutumiwa na watu kwa uhalifu ndipo walipoingia na kujenga.

Aliongeza kuwa baada ya kuanza ujenzi ndipo alipo ibuka Benjamini Mutabagwa na kueleza kuwa ni lake ndipo walipofungua kesi mahakama ya Kimara ambapo alishindwa kupeleka vielelezo vya umiliki wa eneo hilo.

Mwanasheria anayewatetea wananchi hao, Moses Chunga alisema kitengo cha kubomoa nyumba hizo ni kukiuka sheria za mahakama kwani kuna kesi ya msingi namba 188/ 2016 waliyofungua mahakama kuu ya ardhi ambapo walitakiwa tarehe 31 mwezi huu kwenda kuisikiliza lakini wanashangaa kuona nyumba hizo zikibomolewa.

Alisema wananchi hao wanajipanga kudai fidia ya uhalibifu huo na kuwa kabla ya yote wanahitaji kumuona rais kuona wanapata haki yao.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, Yono Kevela alisema kampuni ya ke imevunja nyumba hizo kwa amri ya mahakama na polisi walikuwepo kusimamia zoezi hilo.

"Mwenye eneo hilo ambaye ni Kanisa la Winers alishinda kesi mwaka mmoja uliopita na leo jana ulikuwa ni utekelezaji wa kuwaondoa wavamizi hao" alisema Kevela.

Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamisi alisema kitendo walichofanyiwa si cha uungwana hata kidogo kwani wao wapo katika eneo kwa siku nyingi mpaka wamefikia hatua ya kujenga nyumba hizo hizo mmiliki huyo alikuwa wapi kwa siku zote hizo.

"Kwa kweli hawa watu wanatufanya tusiipende serikali yetu tunaomuomba rais atusaidie katika jambo hili" alisema Hamisi.

Hamisi alisema kesho leo wanatarajia kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Ubungo kupeleka kilio chao na kama akishindwa watakwenda kwa mkuu wa mkoa na kama napo hawatapata ufumbuzi watakwenda kumuona waziri Lukuvi na Rais.

Hawa Musa alisema baada ya kuvunjiwa nyumba zao wapo katika wakati mgumu na hawajui wataisheje na watoto wao.

Alisema wamepanga vitu vyao nje na mvua yote iliyonyesha jana imelowanisha vyombo vyao yakiwemo magodoro na hawajui huyo mtu anayedai ni eneo lake nyuma yake yupo nani.

Alisema nyumba yake iliyobomolewa ilikuwa inathamani ya sh. 700,000.

"Tangua tufungue kesi mahakama ya Kimara hakuwahi kufika kama yupo kweli kwanini anashindwa kuhudhuria mahakamani " alihoji Musa.

Musa aliongeza kuwa kabla ya kubomoa nyumba hizo walipaswa kutoa notsi lakini wao hawajafanya hivyo wamefika saa mbili asubuhi na kuanza kubomoa bila hata ya kuwa shirikisha vipongozi wa eneo hilo.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Juma Abdallah amelalamikia jeshi la polisi kwa kuchukua TV, king'amuzi na sh. 80,000 zilizokuwepo ndani kabla ya nyumba yake kubomolewa.

"TV yangu na king'amuzi na sh.80,000 zimechukuliwa wakati wa zoezi hilo" alisema Abdallah.

 Katika hatua nyingine wananchi hao wamemtupia lawama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tegeta A  kuwa amekuwa akiwakumbatia watu wanaodai kuwa eneo hilo ni lao wakati anaelewa fika ukweli halisi wa eneo hilo.

Mwenyekiti huyo Marko Vaginga alipopigiwa simu ili kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kuzungumza chochote zaidi ya kumtaka mwandishi kwenda ofisini kwake kwa mazungumzo zaidi.

"Nakuomba uje ofisini tuzungumze kwa leo sipo tayari kuzungumza chochote" alisema Vaginga na kukata simu.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alipopigiwa simu alisema polisi walikuwa eneo hilo kwa ajili ya kusimamia amri ya mahakama.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post