UVCCM YATOA SIKU SABA MAALIM SEIF AZUILIWEKUENEZA SIASA MSIKITINI

kaimu katibu mkuu wa UVCCM taifa Shaka Hamdu Shaka
Na Woinde Shizza, Dar es  salaam.
Umoja wa Vijana wa chama cha Mapinduzi umetoa siku saba kwa serikali  ya Mapinduzi Zanzibar  (SMZ ) kuchukua hatua sahihi dhidi ya wanasiasa wanaohubiri siasa kwenye nyumba za ibada vingingevyo UVCCM nayo itaingia mitaani kuuthubitishia ulimwengu kuwa hakuna utii  wala utawala wa sheria visiwani humo.
Umoja huo pia umemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwiguli Nchemba, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Zanzibar Mohd Aboud  na msajili wa vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi kutoka hadharani na kuthibitisha iwapo  kinachofanywa hivi  sasa  na Katibu Mkuu wa CUF  Seif sharif Hamad ni matakwa ya sheria vyama vingi No 5 ya mwaka 1992.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka ameeleza hayo jana alipoongea na waandishi wa habari kufuatilia kauli ya uvccm waliyoitoa hivi karibuni kutahadharisha  juu ya  kitendo cha Maalim Seif kuendelea kuhutubia siasa kwenye nyumba za ibada visiwani humo  huku mamlaka za dola zikiwa kimya na kushindwa kumdhibiti kwa mujibu wa Katiba  na sheria .
Shaka alisema ni mambo ya ajabu sana kumuona mwanasiasa mmoja  akiendelea kuzitumia nyumba za ibada kueneza siasa za chuki bila kuchukuliwa hatua za kisheria huku akitamba mitaani kama kwamba Nchi haina sheria, Katiba wala viongozi dhamana.
"Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais na Msajili wa Vyama Vya Siasa sasa watoke hadharani ili  kuthibitisha iwapo yanayofanywa na Maalim Seif ni matakwa ya sheria ya vyama vingi au ni ubabe wa kisiasa"alieleza Shaka.
Alisema imefika mahali Vijana   hawaelewi kama yupo mwanasiasa ambaye aliye  juu sheria na Katiba hadi afikie kubeza  sheria na taratibu za Nchi bila kuchukukiwa hatua stahiki 
Shaka alisema UVCCM imefika mahali haijui kama yupo  kambare au hongwe, tujuavyo hakuna ushirika katika kuendesha ufalme, ufalme ni mmoja na kila raia anapaswa kuheshimu sheria na vyombo vya dola.
Aidha alieleza kuwa hakuna mtu aliyemshawishi Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif  akilazimishe chama chake kisusie uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu hivyo anapohamishia siasa kwenye nyumba za ibada ni wazi sasa ana mpango hatari wa kuiingiza nchi katika ghasia na machafuko.
"Hivi ni nani Maalim Seif Zanzibar , yeye ana mamlaka yepi hadi akaidi sheria za nchi huku akitazamwa macho , kwa nini anatamba na kufanya atakavyo, viko wapi vyombo vya ulinzi na usalama, wasipotoa majibu muafaka  tutaingia mitaani ili kuyahami Mapinduzi yetu "alisema Kaimu huyo..
Alieleza kuwa Mapinduzi ya januari 12 mwaka 1964 yalioleta manufaa   kwa kizazi cha wakwezi na wakulima  baada ya miaka 50 kupita, haya ni Mapinduzi ya  vijana, yalifanywa na vijana wenzetu na sasa tutayatea   wala si Mapinduzi ya kuchezewa na wasaliti au vibaraka , tutampima kila kiongozi kwa ujasiri au usaliti wake .
Shaka alisema Maalim Seif alihutubia msikitini huko Mbuyuni, akaenda Khinani pia ijumaa iliopita  amehutubia msikiti wa kwa Bi Zired bila vyombo vya ulinzi na usalama wa raia kumchukukulia hatua zozote huku mwanasiasa huyo na wafuasi wake wakijigamba mitaani .
"Uvccm tunaheshimu dhana ya utawala wa sheria ila si washindwa wa kuleta ghasia popote pale, ikiwa waliopewa dhamana za juu wanajivika macho yenye makengeza , hatutasita kuingia barabarani wakati wowote na hapo dunia isije ikatulaumu "alisema shaka
Juhudi za kumpata katibu mkuu wa cuf Maalim Seif , Waziri Mwigulu Nchemba na Mohamed Aboud ziligonga ukuta baada ya simu zao kuita muda mrefu 
bila kupokelewa hadi tukienda mitamboni

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post