MILYA WA UVCCM ARUSHA AUSHUTUMU MGODI WA TANZANITE ONE .


MWENYEKITI wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM(Uvccm),mkoani Arusha,James Ole Milya ameishutumu  kampuni ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite One iliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa madai kwamba imekuwa ikitoa ajira kwa watu wa nje na kuwatupa wazawa huku akisisitiza kuwa   binafsi haoni faida kwa kampuni hiyo kuwekeza wilayani humo.

Pia,ameishauri serikali isitie saini mkataba mwingine na kampuni hiyo pindi utakapomaliza wa sasa  mnamo mwezi  machi mwaka 2012 kwa kuwa  kampuni hiyo imekuwa ikitoa misaada kidogo kwa jamii inayouzunguka mgodi huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa j na Milya kwa waandishi wa habari alisema kuwa pamoja na kampuni hiyo kuwekeza  wilayani  Simanjiro lakini haoni faida tangu iwekeze kwa kuwa hata ajira zimekuwa zikitolewa kwa wageni badala ya wazawa.

Alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa vijana wa Simanjiro ambao  wamekuwa wakidai kukosa  ajira na kubaki maskini huku akisisitiza ya kuwa vijana hao wameshindwa kupewa hata ajira ya kuchimba udongo ndani ya mgodi huo  kwa kigezo cha kutokuwa na elimu.

“Huu ni uonevu mkubwa ni lazima sisi kama wazaliwa na wakazi wa jimbo la Simanjiro tusimame kutetea maslahi yetu,hawa wawekezaji wamewekeza Simanjiro na mimi sioni faida ya kampuni hii kuwekeza   kwani  hata ajira zinatolewa kwa watu wa nje tu lakini si wazawa”

“Hata kama vijana wa Simanjiro hawana elimu ya kidato cha nne kwani kuchimba udongo pia inahitaji elimu ya juu…,hizi kazi wangepewa vijana wa Simanjiro wangekabiliana na umaskini ”alihoji Milya

Milya, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM taifa alisema kuwa yeye kama kiongozi wa jumuiya hiyo  atatumia nafasi yake kuishauri serikali isitie saini mkataba mwingine na kampuni hiyo na ipewe kampuni nyingine itakayojali maslahi ya wananchi wa Simanjiro.

Hatahivyo,aliibua shutuma nzito kwa kampuni hiyo kwamba   imekuwa ikitoa misaada kwa kijiji kimoja pekee badala ya vijiji 54 vilivyopo wilayani humo na kusisitiza kwamba  atapigania maslahi ya wakazi wa vijiji vyote hadi kieleweke.

“Wao wamekazana kutoa misaada ambayo pia haitoshelezi kwa vijiji husika,wanatoa misaada kwa kijiji kimoja tu badala ya vijiji 54 vya jimbo la Simanjiro ambavyo vyote vinahitaji misaada,mimi nasema nitapambana hadi kieleweke bila woga”alisisitiza Milya 

Akijibu malalamiko hayo hivi karibuni ofisini kwake baada ya libeneke hili kuwasili kwa lengo la kuthibitisha taarifa hizo,mwanasheria wa kampuni hiyo,Lusekelo Mwakalukwa alikanusha vikali madai yote yaliyotolewa dhidi ya kampuni yao na kusema kuwa wametoa misaada mingi na kuajiri watumishi wengi ambao ni wakazi wanaouzunguka mgodi huo.

Mwakalukwa,aliitaja misaaada mbalimbali iliyotolewa na kampuni yao na kusema kuwa misaada hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule ya msingi iliyopo ndani ya kata ya Naisinyai,ujenzi wa barabara kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA hadi mgodini pamoja na huduma za afya hususani kliniki za macho.

Aliitetea kampuni hiyo kuhusiana na kero za ajira kwa wazawa na kusisitiza ya kuwa  pamoja na yeye binafsi kutokuwa na idadi ya ajira hizo zilizotolewa kwa wakazi hao lakini alidai kuna  idadi kubwa ya wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi lakini wamepatiwa ajira bila ya ubaguzi.

“Mimi sio meneja uajiri sina statistics(takwimu),lakii kuna watu wengi sana tumewaajiri bila hata ubaguzi,sisi hatuna ubaguzi kwenye masuala ya ajira na misaada hii ni vitu viko wazi kabisa”alisema Mwakalukwa

Hatahivyo,aliemba mbali zaidi na kudai ya kuwa kampuni yao imekuwa ikilipa kodi kwa  utaratibu mzuri na kusisitiza ya kuwa kampuni yao imekuwa ikitoa misaada kulingana na uwezo wa kifedha kwa kuwa kampuni yao inategemea fedha kupitia biashara ya madini aina ya Tanzanite.

“Tunalipa kodi kwa utaratibu,tunatoa misaada kw auwezo tulionao so far(mbali zaidi) tunategemea pesa zaidi na tutaoa misaada mingi tu”alisisitiza Mwakalukwa


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post