BREAKING NEWS

Tuesday, December 27, 2011

UZEMBE WA MADAKTARI WACHANGIA MAMA MJAMZITO KUFARIKI DUNIA


HOSPITALI teule ya jiji la Arusha,Saint Elizabeth imeingia katika kashfa nzito baada ya kudaiwa kusababisha kifo cha mama mjamzito Mary Lukas Mollel(36) na mtoto wake kutokana na kilichoelezwa kuwa ni uzembe wa watumishi wa hospitali hiyo.

Mme wa marehemu, Daudi Moruo Mollel ambaye ni mkazi wa Kisongo wilayani Arumeru akieleza kwa masikitiko alisema mke wake alifika hospitalini hapo siku ya jumatano na alikuwa akiwasiliana nae hadi siku ya ijumaa usiku alipozidiwa na kuaga dunia.

Alisema kabla ya kifo cha mke wake alimwambia kuwa alikuwa amepewa dawa za kumwongezea uchungu huku kukiwa hakuna daktari karibu wa kumhudumia hali iliyosababisha kutokwa na damu nyingihadi mauti yalipomkuta.

“Ninavyofahamu mama mjamzito anapopewa dawa za kumwongezea uchungu lazima daktari awe karibu,lakini usiku walikuwepo wauguzi  tu,ambao hawakuweza kuokoa maisha yake na mtoto,huu ni uzembe ambao hatuwezi kuufumbia macho.”alisema Mollel

Alisema mke wake ambaye alikuwa  mwalimu wa shule ya msingi Kipok wilayani Monduli,alitarajiwa kujifungua Novemba 30,mwaka huu na kilichotakiwa baada ya kufikishwa hospitali  Desemba 22, jambo lililotakiwa ni kufanyiwa upasuaji haraka lakini hawakufanya hivyo.

Naye kaka wa marehemu Abel Lukas Mollel mkazi wa Olasiti mjini Arusha, alilaumu huduma za hospitali hiyo kusababisha kifo cha ndugu yake na mtoto kuwa hapakuwa na umakini wa kutosha katika kuwahudumia  na kusababisha vifo vyao.

“Tumehambiwa na  wagonjwa aliokuwa amelazwa nao kuwa ndugu yetu alihangaika sana akipiga kelele za kuomba msaada lakini hakupata msaada kwa wakati,baada ya kutokwa na damu nyingi walijaribu kumwongezea damu lakini haikusaidia.”alisema Mollel

Jitihada za kuonana uongozi wa hospitali hiyo hazikufanikiwa kwa madai kuwa mganga mkuu wa jiji ndiye mzungumaji.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates