BREAKING NEWS

Tuesday, December 6, 2011

TANZANIA NI NCHI YA NNE KATI YA 50 KWA UKATILI WAWANAWAKE

IMEELEZWA kuwa katika ukatili unaofanyika kila siku dhidi ya wanawake,Tanzania ni nchi ya nne kati ya nchi 50 duniani,ambazo zina kiwango kikubwa zaidi cha ukatili kwa wanawake majumbani.

Hayo yalisemwa  na David Ntiruka,Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Haki Madini,ya mji mdogo wa Mirerani,wilaya ya Simanjiro,mkoani Manyara inayoendesha kampeni ya tunaweza kuzuia ukatili dhidi ya wanawake.

Alisema kiwango cha ukatili nchini ni kikubwa zaidi na waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana na inakadiriwa kuwa,mmoja kati ya wanawake wanne Tanzania,wapo katika hatari ya kufanyiwa ukatili.

Ntiruka alisema ili kushiriki wiki ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake duniani Haki madini,wataendesha kampeni hiyo kwa muda wa siku tano ambapo zilianza jumatatu iliyopita na zitafikia kilele ijumaa ya Desemba 2 mwaka huu.

Alisema katika kilele cha maadhimisho hayo,mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Ofisa maendeleo ya jamii wa mji mdogo wa Mirerani,Issaya Mgaya na watu zaidi ya 300 wanatarajia kushiriki katika kampeni hiyo.

Alisema asilimia 56 ya wanawake nchini wanaona ukatili ni sehemu ya maisha yao na asilimia 60 ya wanawake waliofanyika ukatili hawakutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

“Wanawake duniani kote wanakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii ikiwemo ukatili majumbani hali inayowaumiza kimwili,kubakwa,kutukanwa, kunyanyaswa na kudhulumiwa mali zao za ndoa,” alisema Ntiruka.

Alisema hapa nchini,matendo ya ukatili yamejikita katika mila na desturi taratibu,tamaduni na mifumo ya kikandamizaji ambayo humchukulia mwanamke kuwa ana hadhi ya hali ya chini.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates