JUMLA ya kiasi cha $ 60,000,000 zimetolewa na shirika la misaada la kimarekani la USAID hapa nchini kwa lengo la kuinua sekta mbalimbali za kilimo na miundombinu kama njia ya kupunguza na kutokomeza janga la umaskini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kiongozi wa timu ya kilimo na chakula kupitia shirika hilo,Thomas Hobgood alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na shirika hilo hapa nchini kwa awamu ya kwanza kama njia mojawapo ya kuinua sekta binafsi hususani kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo wadogo.
Akihojiwa na waandishi wa habari katika mkutano wa wadau wa sekta ya maendeleo kutoka zaidi ya nchi 100 duniani uliofanyika jijini hapa,Hobgood alisema kuwa shirika lao limejikita kusaidia katika kuweka mazingira mazuri kwa wakulima hapa nchini.
Alisema kuwa shirika lao limeanza na utaratibu wa kuwasaidia wakulima kutoka mikoa ya Morogoro,Manyara,Dodoma na Zanzibar katika kuwawezesha kwa kama njia mojawapo ya kuboresha sera ya kilimo kwanza hapa nchini.
“Tumeamua kusaidia hii programu ya kilimo kwanza ndani ya shirika letu kwa kuanza na mikoa niliyoitaja kama njia ya kutokomeza umaskini nah ii ni awamu ya kwanza”alisema Hobgood
Alibanisha ya kuwa wamejipanga kuwawezesha wakulima kutoka mikoa hiyo kulima mazao ya mchele na mahindi kwa kiwango cha asilimia 50 hali ambayo itasaidia kutokomeza tatizo la njaa na lishe duni linaloikabili Tanzania.
Hatahivyo,alisisitiza ya kuwa endapo Tanzania itajikita kuboroshea mazingira mazuri ya sekta ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo mbalimbali kuna uwezekano mkubwa wa kutokomeza umakini na kuharakisha maendeleo kwa haraka.