TPC YAJENGA UKUMBI WA KIMATAIFA

KAMPUNI ya sukari ya TPC ya wilayani Moshi imejenga ukumbi mpya wa
kisasa wenye uwezo wa kuchukua watu 1200 utasaidia watu binafsi
,makampuni na taasisi
mbalimbali kufanyia mikutano yao mikubwa..

Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi huo unaojitoshereza kwa
kila kitu serikali mkoani humo imesema itahamishia mikutano yake yote
mikubwa katika ukumbi huo kutokana na hali ya utulivu iliyopo katika
eneo hilo.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro
Leonidas Gama wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa TPC ,ulioenda sanjari na
sherehe ya kuwaaga wastaafu wa kiwanda hicho wa mwaka 2011.

“Niwapongeze waliobuni wazo la kuwa na ukumbi wa kisasa kama
huu…hatukujua mapema majuzi waziri mkuu amekuja kututembelea
tukalazimika kwenda kubanana katika ukumbi mdogo ,lakini tungejua
mapema tungemleta waziri mkuu kufanyia mkutano wake hapa”alisema Gama.

Alisema mbali na mikutano ukumbi huo pia utaweza kutumika kwa ajili ya
burudani kwa viongozi ambao wangependa kucheza dansi wakati mwingine
lakini wamekuwa wakishindwa kufanya hivyo kutokana na kwamba kulikuwa
hakuna ukumbi ambao ungewawezesha na wao kupata burudani.

“Wakati mwingine viongozi pia wanataka kujitikisa kidogo lakini
walifikiri wapi waende,ukienda kujichanganya kwenye kumbi zetu za
mjini,wataulizana hee na huyu nae vipi ?sasa tutaweza kuja hapa mara
moja moja”alisema Gama

Kwa upande wake afisa mtendaji mkuu wa TPC ,Robert Baisaac alisema
uwepo wa jengo hilo utaongeza ubora wa maisha ya wakazi wa TPC ,
vijiji jirani na mji wa Moshi kwa kutumia ukumbi huo kwa matukio
tofauti yatakayofanyika katika ukubi huo.

“Tutapenda kuona jingo hili likitumika kwa burudani kila wiki
,tutapenda kuona matamasha,sanaa  za maonesho ,muziki,ngoma za
utamaduni,maonesho ya sinema yakifanyika hapa”alisema Baisaac.

Alisema ukumbi huo ni mfano hai wa kuwa wanahisa na bodi ya
wakurugenzi wanathamini ustawi wa wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na
kuboresha mazingira ya TPC kwa manufaa ya wafanyakazi.

Ujenzi wa ukumbi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 500 ulianza
Februari 21 mwaka huu chini ya mkandarasi Kalsi & Jutley Enterprises
na kukamilika Novemba 19 mwaka huu.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post