POLISI mkoani Manyara kwa kushirikiana na wasamaria wema wamefanikiwa kukamata kundi la Raia 18 wa Ethiopia na Somalia wilayani Kiteto wakiwemo watanzania wawili waliokuwa wakiwasaidia katika jaribio la kuwavusha nchini kinyemela kuelekea nchini Malawi.
Aidha kati ya raia hao miongoni mwao wapo wafanyabiashara wawili wa Somalia mkazi wa wilayani Tunduma mkoani Mbaye na Ethiopia mwenye makazi yake jijini Nairobi Kenya wanaodhaniwa kuwa sugu kuhusika katika biashara hiyo kinyemela kwa kushirikiana na watanzania wawili wakazi wa jijini Arusha ambao wanatuhumiwa kuitumia wilaya ya Simanjiro kama mapitio yao.
Hivi karibuni mkuu wa wilaya ya Simanjiro hiyo Khalidi Mandia wakati akifunga mafunzo ya wanamgambo 186 katika kata ya Loibosiret tarafa ya Emboret alikiri wilaya hiyo kutumiwa na wananchi wachache kuwapitisha raia wa nchini hizo na kuwataka wananchi kwa kushirikiana na mgambo hao kuchukua tahadhari ya kukabiliana na kikundi cha Alshabaab cha nchini Somalia.
Akizungumzia mazingira ya ukamataji kamishna msaidizi wa polisi mkoani hapa Liberatus Sabas alikiri kukamatwa kwa kundi hilo Novemba 26 saa 3:00 usiku katika kichaka ambacho kundi hilo lilihifadhiwa ili wafanyabiashara hao waweze kuangalia mwelekeo wa kuwavusha kabla ya wasamaria wachache kufichua kundi hilo na kutiwa mbaroni.
“tumewakamata lakini kundi kubwa ni wahabeshi waliokuwa wakivushwa kwa kushirikiana na watanzania na raia wawili wa Somalia na Ethiopia…sasa tunafanya jitihada za kuwasafirisha ili leo(jumatano) waweze kusafirishwa na kufikishwa mahakamani leo(alhamisi)…hawa wote wamekiuka sheria lazima tuwashtaki”alisema Sabas.
Aliwataja watanzania wawili walioamatwa wakishirikiana na raia hao wa Somalia na Ethiopia wenye makazi yao wilayani Tunduma kuwa kuwa ni Rashidi Bakari(34) na mkazi wa Engarenarok Kiteto na jijini Arusha na Hamisi Hosseni(50) wa jijini Arusha,huku wenyeji wanaotuhumiwa kujihusisha na raia hao kuwa ni Makassy Ali(34) mkazi wa Tunduma raia wa Somalia na Selasie Ibrahim(18) raia wa Ethiopia mkazi wa Nairobi Kenya.
Akifafanua kukamatwa kwa raia waliokuwa wakivushwa alisema siku hiyo majira ya saa 2:30 usiku mjini Kibaya wilayani kiteto walipata fununu ya kuwepo kwa lori aina lenye namba za usajili T284 AHW lililokuwa likiendeshwa na Rashidi Bakari mali ya kiongozi wa msafara huo Haruna Hosseni likiwa eneo la wilaya ya Simanjiro toka jijini Arusha kuelekea wilayani Kiteto.
“polisi walipopata taarifa hizo waliweka mtego uliofanikisha kuwanasa wahabeshi hao waliokuwa wamefichwa..tuliwakamata dereva na kiongozi raia wa Somalia mkazi wa Tunduma tulipowahoji walikiri kulificha kundi hilo ambalo lilikuwa likielekea mkoani Mbeya tayari kwa kufanya mipango ya kuwavusha kuelekea nchini Malawi”
“wote 18 tumewakamata na kuwakabidhi jeshi la uhamiaji..watanzania wawili hao watashughulikiwa kisawasawa kwa kushikiriana nao hao wahabeshi na wasomali…sisi tunawataka raia wachukue tahadhari na kuwafichua..wenzetu wao ndio wanajishughulisha na biashara hiyo..sasa wanaletwa hapa babati ili kuwafikisha mahakamani”
Hata hivyo Sabas alipoulizwa kwanini kumekuwepo na mwanya katika barabara hiyo licha ya jeshi hilo kutoa kauli zake mara kadhaa kuwa limeimarisha ulinzi katika eneo la barabara hiyo wilayani Simanjiro inatumiwa mara kwa mara kuvusha raia wa Somalia alisema baadhi ya watanzania wamekuwa wakitumia njia za panya kuwapitisha raia hao kama sehemu ya kufanikisha biashara yao.
Pamoja na kuwapongeza raia hao bado amewataka wananchi kuipenda nchi yao kwa kuwafichua raia hao wa Somalia pindi wanapopitishwa kwenye malori na wengine wanaowatilia shaka ikiwa pia ni njia itakayoweza kukidhibiti kikundi cha mtandao wa Alshabaab ambacho kimekuwa tishio nchini Kenya.
Kwa upande mwingine baadhi ya wananchi wameitaka serikali kufichua mtandao wa baadhi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji wa raia hao uliopo jijini Arusha unadaiwa kufanya biashara hiyo kwa gharama ya dola 100 kwa kila raia ambao kama usipodhibitiwa huenda ukashirikiana na kikundi cha Alshaabab chenye mtandao wake nchini Somalia