KWAKIPINDI CHA MWEZI MMOJA MADIWANI 60 WAJIUNGA NA CCM



Wakati vuguvugu la madiwani kujiuzulu nyadhifa zao likiendelea kuchukua sura mpya siku hadi siku, imebainika kwamba tangu Januari mwaka juzi hadi sasa, kata 89 ziliondokewa na madiwani wake kwa sababu mbalimbali, ikiwamo vifo, kutenguliwa mahakamani na kujiuzulu.

Uchunguzi umebaini kuwa katika idadi hiyo, madiwani 60 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamejiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Madiwani hao walijiuzulu na kufuata uanachama wa CCM kwa hoja kwamba wanaunga mkono utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli.

Mbali na idadi hiyo, madiwani watano wa Chadema na mmoja wa CCM walitenguliwa na mahakama katika nyadhifa zao.

Katika orodha hiyo, pia kata 23 zilibaki wazi baada ya madiwani waliokuwa wakiziongoza kufariki dunia.

Ndani ya orodha ya madiwani 23 waliofariki dunia, 19 walikuwa wa CCM, wawili Chadema, mmoja ACT-Wazalendo na mmoja CUF.

Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Tume ya Uchaguzi (NEC), Clarence Nanyaro, ameliambia gazeti hili kwamba hadi Februari 17, mwaka huu, kata 82 zilishafanya uchaguzi kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post