Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema
kimeridhishwa na matumizi ya Sh500milioni zilizotolewa na Serikali katika
halmashauri 183 nchini kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo mapya ya
zahanati na vituo vya afya.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 25, 2018
na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole wakati
ikikagua ukarabati unaoendelea katika kituo cha afya cha Usa-River halmashauri
ya Meru wilayani Arumeru mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kutembelea
kaya masikini zilizowezeshwa na mfuko wa Tasaf
"Mnafanya kazi
nzuri inaendana na kiwango cha ubora wa miradi na kile cha fedha
zinazotolewa ambazo zinatokana na kodi za Watanzania,” amesema.
Mganga mkuu wa wilaya, Cosmas Kilasara
amesema miradi ya wilaya hiyo inaendelea vyema na kuwanufaisha wananchi.
Miradi hiyo ilitambulishwa katika kikao cha
menejimenti ya halmashauri (CMT), kikao cha kamati ya elimu, afya na maji na
kikao cha kamati ya fedha, uongozi na mipango
Amesema Februari mwaka huu mradi huo
ulitambulishwa kwenye baraza la madiwani na kazi kuanza kufanyika kwa ujenzi wa
majengo mapya likiwemo jengo la upasuaji mkubwa.
Majengo mengine ni pamoja na maabara, wodi
ya mama na mtoto, nyumba ya mtumishi inayojitegemea, jengo la kufulia, jengo la
kuhifadhia maiti, tanki la kuhifadhia maji, tanuru la kuchomea taka pamoja na
njia za kuunganishia majengo ambayo yote yapo katika hatua mbalimbali za
utekelezaji wake
Aidha alitaja mradi huo kuwa unahusisha pia
ukarabati wa majengo likiwemo jengo la wagonjwa wa nje, wodi ya wazazi, duka la
dawa na jengo la utawala ambayo bado utekelezaji wake haujaanza.
Alisema hadi kufikia Februari 23 mwaka huu
jumla ya Sh135.4 milioni zilikuwa zimeshatolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa
mbalimbali vya ujenzi na sehemu za gharama za ufundi.
Amesema pamoja na kiasi hicho cha fedha upo
pia mchango wa nguvu kazi kutoka kwa wananchi wa kata ya Usa-River pamoja na
vijana wa CCM kwa kuchimba misingi ya majengo ya maabara na jengo la nyumba ya
mtumishi pamoja na kukusanya mawe unaofikia Sh1.2 milioni.