Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti
amewaagiza wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuwalipa mishahara
wachimbaji na wasipotimiza hilo wasitishe shughuli hizo
Mnyeti amesema hayo leo Februari 25,2018
alipozungumza na wamiliki wa migodi, mameneja na wachimbaji katika mji mdogo wa
Mirerani wilayani Simanjiro
Amesema utekelezaji wa agizo lake unapaswa
kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hakuna mjadala
katika utekelezaji kwa kuwa kwa muda mrefu wamiliki wa migodi wanajinufaisha
wao na familia zao bila kujali haki za wachimbaji
Mmoja wa wamiliki wa migodi, Abubakary
Madiwa amesema suala la kuwalipa mishahara wachimbaji litakuwa gumu kutekelezwa.
Madiwa amesema endapo hilo litafanyika ni
wamiliki wapatao 10 watakaokuwa na uwezo wa kulipa mishahara wafanyakazi
wao.
"Ni bora ungesema migodi ifungwe kuliko
kutuagiza tuwalipe mishahara wachimbaji hawa kwa kuwa tuna utaratibu wa
kuangalia haki zao pindi uzalishaji unapofanyika," amesema Madiwa
Mnyeti akijibu hoja ya Madiwa amesema, "Kama wewe huwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi wa migodini ufungashe virago urudi nyumbani, ukatafute kazi nyingine ya kufanya,
Sheria haina huruma, mama mjane au mwanamke
ni kule nyumbani huku machimboni anakuwa mkurugenzi wa mgodi, sina huruma kwa
hilo walipeni mishahara wafanyakazi wenu," amesema
Kaimu katibu tawala mkoa, Missaile Mussa
amesema wachimbaji wa madini wanapaswa kulipwa mishahara kwa mujibu wa sheria
ya kazi namba sita ya mwaka 2004.
Mussa amesema wachimbaji wanastahili
kupatiwa mishahara na stahili zao kama wafanyakazi wengine.