MAHAKAMA YAAGIZA NABII TITTO APIMWE UPYA AKILI




MAHAKAMA ya Wilaya ya Dodoma imeagiza mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma Tito Machibya, maarufu kama ‘Nabii Tito’ (45) kupimwa akili upya katika Taasisi ya Afya ya Akili ya Mirembe Isanga mkoani Dodoma ili kujiridhisha kama ana matatizo ya akili.

Licha ya kuagizwa mtuhumiwa huyo kufanyiwa vipimo upya, mahakama pia imetaka kuwasilishwa kwa vielelezo kama kweli ana tatizo hilo kama alivyoieleza mahakama.

Nabii Tito anashtakiwa kwa kosa la kujaribu kujiua kwa kutumia wembe.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, alisema jana kuwa kutokana na mshtakiwa kuieleza mahakama kuwa ana matatizo ya akili na alifanya tukio hilo kutokana na kusikia vitu ambavyo vilikuwa vinamwamuru akate, mahakama itabidi ipate vielelezo ambavyo vitathibitisha anachokisema.

Karayemaha alisema kutokana na kifungu namba 219 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kama mshtakiwa atabainika kweli ana matatizo ya afya ya akili, mahakama itaamua kuwa alivyofanya tukio hilo hakuwa na akili timamu, hivyo hana hatia.

“Mshitakiwa anadai kuwa ana matatizo ya akili na amekuwa akitibiwa katika hospitali mbalimbli ikiwemo ya Maweni. Mahakama hii inaagiza vielelezo vyake vyote viletwe hapa lakini pia apelekwe kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili Mirembe Isanga,” alisema Karayemaha.

Pia alisema kama mshtakiwa atabainika kuwa hana tatizo lolote la afya ya akili kwa mujibu wa vielelezo vyake pamoja na vipimo atakavyofanyiwa, atakuwa na kesi ya kujibu.

“Kutokana na hili aliloiambia mahakama kuwa ana matatizo ya akili hata suala la dhamana tunaliweka pembeni kwanza kwa sababu hawezi kujieleza lakini kama itabainika kuwa hana matatizo ya akili kutokana na vielelezo vitakavyoletwa pamoja na vipimo vitakavyofanyika, suala la dhamana litafanyiwa kazi,"alisema.

Hata hivyo alisema mshtakiwa huyo anarudi rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa Februari 19, mwaka huu.

Wakati kesi itakapotajwa vielelezo vyote pamoja na vipimo vinatakiwa kuwa tayari vimeshawasilishwa mbele ya mahakama hiyo.

Nabii Tito anashtakiwa kwa tuhuma za kutaka kujiua kwa kujikata

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post