Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akijibu maswali bungeni Mjini Dodoma
Na
Mathias Canal, Dodoma
Serikali imesema kuwa Zoezi la
upokeaji na usambazaji wa viuwadudu linaendelea na hadi kufikia tarehe 24
Januari, 2018 jumla ya chupa 1,733,139 za viuwadudu zimekwisha kusambazwa kwa
wakulima na chupa nyingine 7,287,216 zitaendelea kusambazwa kati ya sasa
na mwezi Machi, 2018 ili kukidhi
mahitaji katika msimu huu wa kilimo.
Hayo yamebainishwa leo 8 Februari
2108 na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akijibu Swali la Mhe
Khadija Hassan Aboud Mbunge wa Viti Maalumu Zanzibar aliyetaka kufahamu namna
ambavyo serikali imejipanga kukidhi mahitaji ya viuwadudu kwa wakulima wa Pamba
nchini.
Alisema kuwa Katika Msimu wa Kilimo
2017/2018 wakulima wameitikia kwa vitendo azma ya Serikali ya kuimarisha kilimo
cha pamba nchini kwa kuongeza eneo linalolimwa pamba kutoka wastani wa ekari
1,000,000 hadi wastani wa ekari 3,000,000, Kutokana na mwitikio huo, hadi tarehe
22 Desemba, 2017 jumla ya ekari 1,500,000 zilikuwa zimelimwa na kupandwa zao la
Pamba na kuhitaji chupa (acrepacks) 4,500,000 za viuwadudu.
Alisema, kwa kuwa mvua zinaendelea
kunyesha wakulima wameendelea kupanda pamba ambapo hadi tarehe 24 Januari 2018
taarifa zinaonyesha kuwa jumla ekari 3,006,785 zimelimwa pamba ambapo Kutokana
na eneo hilo kulimwa pamba, makisio ya chini ya uzalishaji wa pamba ni kilo milioni
600 sawa na tani 600,000 za pamba.
Eneo lote lililo limwa pamba
linahitaji jumla ya chupa 9,020,355 za viuwadudu zenye thamani ya shilingi
bilioni 36 ambapo Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania imenunua jumla ya
chupa 5,300,000 na Kampuni binafsi zimenunua chupa 450,000.
Aidha, jumla ya vinyunyizi vipya
16,500 vimenunuliwa ambapo kati ya vinyunyizi hivyo 10,157 vimekwisha
kusambazwa kwa wakulima na usambazaji unaendelea huku vinyunyizi 6,000 vikiwa
vimekarabatiwa ili kutosheleza mahitaji ya wakulima.