MWIGULU:MIKOA YA KASKAZINI INAONGOZA KWA WAHAMIAJI HARAMU


Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amelitaka jeshi la polisi kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwamba taasisi hiyo ndiyo inayoshughulika na haki za watu na wasipofanya kwa uadilifu yapo madhara makubwa kwa jamii na kutoka kwa wahalifu.


Akizungumza  katika uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha polisi Wilaya ya Pangani jana, Dk Mwigulu alisema kuwa wilaya ya Pangani ni lango ambalo wahalifu hasa wahamiaji haramu hupitia kwenda kusini mwa Tanzania.

‘’Kamateni wahalifu wote wanaoingia kimagendo au wanaoingiza mizigo kimagendo hakuna mjadala kamateni na wafikisheni katika vyombo vya sheria ,’’alisema Dk Mwigulu.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, Mikoa ya kaskazini mwa Tanzania inaongoza kwa kuingiza wahamiaji haramu na bidhaa kwa magendo kwasababu ipo mipakani hivyo kuamua kuchangia vifaa vya ujenzi ili kuunga mkono juhudi hizo.

‘’Ujenzi huu wa kituo cha polisi utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama zaidi hivyo mimi nitachangia nondo 150 baada ya mifuko 450 ya cement kupatikana basi ujenzi uanze haraka iwezekanavyo na kituo kiwe cha hali ya juu kikubwa.’’ alisisitiza

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi wilaya hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa polisi Christina Musyani amesema kuwa wilaya hiyo ina vituo vitatu pekee vya polisi ambavyo havitoshi na mazingira yake hayaridhishi.

Alisema wameamua kuanza ujenzi wa kituo hicho ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa sasa hulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta vituo vya polisi.

"Kwa kushirikiana na wananchi, Mbunge na halmashauri tumeamua kuanza ujenzi wa kituo cha kisasa ,’’ alisema Christina.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post