Ikiwa kwenye msimu wake
wa kwanza tangu irejee ligi kuu klabu ya Singida United, imezidi kuonesha njaa
ya vikombe kwenye msimu wake wa kwanza, baada ya leo kufanikiwa kushinda mchezo
wake wa FA dhidi ya Polisi Tanzania.
Mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja
wa Namfua mjini Singida jioni ya leo, Singida United imeibuka na ushindi wa
mabao 2-0 hivyo kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa
wake anapata nafasi ya kuwakilisha nchi.
Mabao ya Singida United jioni ya leo
yamefungwa na Juma Kennedy dakika ya 70 pamoja na Tafadzwa Kutinyu dakika ya 77
na kuimaliza Polisi Tanzania ambayo imesafiri kutoka jijini Dar es salaam.
Singida United sasa imekuwa timu ya
pili kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya shirikisho, ikitanguliwa
na Njombe Mji ambayo ilifuzu kwa kuiondoa timu ya Mbao FC ambayo ilicheza
fainali msimu uliopita na kupoteza mbele ya Simba.
Baadae kuna mchezo mwingine wa 16
bora, Azam FC watakuwa nyumbani kwao Azam Complex kucheza na KMC ya Kinondoni.
Yanga wenyewe watashuka dimbani kesho dhidi ya Majimaji ya Songea.