Mohammed Enterprises yazindua shindano la Pindua Ushinde

Mohammed Enterprises yazindua shindano la Pindua Ushinde
Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) imezindua shindano la Zawadi ya Chini ya Kizibo (UTC) la “Pindua Ushinde” litakalofanyika kwa muda wa siku 45, linalotarajiwa kuisha Machi 10 mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa shindano hilo, Mkurugenzi wa Masoko MeTL, Fatema Dewji ameeleza namna ya kushiriki shidano hilo, kwamba ili ujishindie zawadi, inatakiwa kununua maji ya Mo Maisha na Masafi yenye ujazo kuanzia Mili lita 600 hadi lita 1.7.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania tunawaletea shindano la zawadi ya chini ya kizibo kwa bidhaa za maji. Hii ni kwa maji ya Mo Maisha na Masafi yenye ujazo kuanzia Mili Lita 600, lita 1 na lita 1.7 ambazo huja kwako katika chupa za plastiki. hii haijawahi kutokea popote nchini Tanzania,” amesema.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Fatema Dewji akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa shindano la Zawadi ya Chini ya Kizibo (UTC) la “Pindua Ushinde”
Amesema, Pindua Ushinde inakupa fursa ya kujishindia zawadi ya Maji ya bure au pesa taslimu kuanzia Sh. 1,000 hadi 100,000, ambapo ili kujionea ulichoshinda, unatakiwa kupindua kizibo cha chupa ya maji ya Mo Maisha au Masafi.
“Maji ya Mo Maisha na Masafi ni safi na salama kwa afya yako na hutayarishwa katika mazingira bora ya usafi wa hali ya juu. Pia,chupa zetu ni safi na salama zilizorafiki kwa matumizi yako zimetengenezwa ili kukidhi viwango vya kimataifa. Kumbuka unapokunywa maji yetu unajiepusha na magonjwa yanayoenezwa kwa maji yasiyo safi na salama,” amesema.
Vile vile, Fatema Dewji amezindua Kampeni ya kutunza mazingira inayofahamika kwa jina la “Tanzania Safi” iliyolenga kuhakikisha ardhi haiharibiwi kwa uchafu wa chupa za plastiki.
“Tutatoa ushirikiano kuondoa chupa za plastiki zitakazoonekana mitaani ili zitumike kama malighafi katika uzalishaji viwandani. Hii si mara ya kwanza kufanya kampeni za utunzaji mazingira, awali MeTL ilifanya kampeni ya utunzaji mazingira kwa kusafisha ufukwe wa Coco Beach," amesema na kuongeza.
“Pia tuliendesha kampeni ya kuelimisha jamii namna ya kuepuka magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama ambapo wataalamu wa afya walielimisha jamii.”
Naye Meneja Mauzo wa Kiwanda cha A 1 kilicho chini ya MeTL kinachozalisha Maji ya Mo Maisha na Masafi, Godfrey Mangungulu amesema washindi wa maji bure na fedha kuanzia 1,000 hadi 50,000 watapewa zawadi zao waliponunua maji, na watakaoshinda zaidi ya fedha hizo watachukua bidhaa zao kwenye Kiwanda cha A1 kilichopo Kurasini.
“Tumeamua kurudisha fadhila kwa jamii, kwa zaidi ya miaka 20 tunauza bidhaa zetu , hivyo tumeamua kurudisha sehemu ya mauzo ya bidhaa zetu kwa jamii. MeTL tuajivunia bidhaa bora na usambazaji wetu unafika nchi nzima,” amesema.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post