Na Woinde Shizza,Arusha
CHUO
cha ufundi Arusha, ATC, kinatarajiwa kukamilisha matengenezo ya
Helkopita na kuirusha angani mapema mwaka 2018 na kuwa ni chuo cha
kwanza nchini kurusha Helkopita iliyotengenezwa na Mhandisi mzawa.
Hayo
yameelezwa jana na Mhandisi wa ufundi aliyebuni na anayetengeneza
Helkopita hiyo, Abdi Mjema, kwenye hafla ya chuo hicho kukabidhiwa
maabara ya maji mwendo ambayo imejengwa na serikali ya Japan,kupitia
shirika lake la misaada la JICA, chuoni hapo.
Mhandisi
Mjema ,amemwambia katibu mkuu wa wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,
Maimuna Tarishi, kuwa matengenezo ya Helkopita hiyo ambayo ameibuni
yamefikia asilimia 40, na anafanya matengenezo hayo kwa kuwasiliana na
mamlaka ya viwanja vya ndege kwa kila hatua anayofikia.
Amesema
hatua ya majaribio ya kuirusha Helkopita hiyo ambayo inatengenezwa kwa
malighafi za nchini anatarajia kuyafanya wiki tatu zijazo mara baada ya
kukamilisha hatua iliyopo sasa ambapo ni 40% ya matengenezo na ambapo
utengenezaji wa Helkopita hiyo anatarajia kuukamilisha mwishoni mwa
mwaka 2017 .
Mjema,
ambae ni mtaalamu wa mitambo aliyebobea pia mhadhiri wa chuo hicho cha
serikali cha ufundi,amesema wazo hilo la kubuni Helkopita hiyo aliibua
kutokana na changamoto za usafiri zilizopo nyumbani kwao wilayani
Mwanga, ambayo eneo kubwa ni milima na wakati wa masika maeneo mengi
huwa hayafikiki.