JIJI LA ARUSHA LAKABILIWA NA TATIZO LA UHABA WA VIWANJA VYA MICHEZO

Picha maktaba uwanja wa sheik Amri Abeid
Na Woinde Shizza, Arusha

JIJI la Arusha linakabiliwa na uhaba  mkubwa wa viwanja vya michezo
hali inayochangia timu nyingi kushindwa kufanya vizuri kutokana na
kutokuwa na eneo maalumu la kufanyia mazoezi.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa ligi ya kombe la vijana la Sakina
,Musa Giriba wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa ligi hiyo
inayoshirikisha timu 14 zinazocheza ambapo fainali watapatikana
mshindi wa kwanza hadi wa tatu michezo  inayofanyika katika viwanja
vya shule ya msingi Ngarenaro.

Alisema kuwa,jiji la Arusha kuna timu nyingi zenye mwamko na
zinazopenda michezo ila changamoto inakuja kwenye viwanja vya kufanyia
mazoezi hali inayowafanya vijana wengi kukata tamaa.

Giriba alisema kuwa, kombe hilo la vijana la Sakina linalenga
kuwasaidia vijana kuona umuhimu wa kupenda masomo na kutumia muda wao
mwingi kwenye mazoezi na kuondokana na makundi yasiyofaa ikiwemo ya
uvutaji wa madawa ya kulevya.

Alisema kuwa, pamoja na kujitahidi kuwaweka vijana pamoja na kuunda
timu hizo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa
vya michezo ikiwemo jezi,mipira na nyavu,hivyo aliomba wadau
mbalimbali kujitokeza kusaidia timu hizo .

‘kwa kweli timu nyingi zinafanya vizuri sana na zinapenda kuendelea
mbele zaidi ila tuna changamoto ya wafadhili wa timu zetu ,kwani mpaka
sasa hivi hatuna wafadhili na tunajiendesha wenyewe kwa kusuasua
,hivyo tunaomba wadau watusaidie ili tufanye vizuri zaidi’alisema
Giriba.

Alitaja timu hizo zinazocheza kuwa ni Town Centre FC,Chinga
City,Sakina youth , Kali Star, Gaza Fc,Kivalovumba,Esso Star,Baston
Fc,Kim Power,Weekend , Morris ,Kilombero Star ,Pentagon na Mchichi Fc.

Naye Afisa michezo wa jiji la Arusha , Benson Maneno alisema kuwa
kutokana na changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ya viwanja vya
mipira  wamejipanga kutengeneza uwanja wa shule ya sekondari Arusha
ambapo tayari wametenga bajeti shs 70 milioni.

Maneno alisema kuwa,fedha hizo ni kwa ajili ya kutengeneza uwanja huo
ili timu zote ziweze kushiriki na kufanya mazoezi muda wote na
hatimaye kukuza na kuinua vipaji vya wanamichezo  jiji la Arusha .

Alisema kuwa,wanasubiri bajeti hiyo ipitishwe mwaka wa fedha mwezi wa
7, ambapo aliahidi kuipatia timu hiyo nyavu za magoli na mipira minne
wakifika nusu fainali.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post