BENKI ZOTE HAPA NCHINI ZATAKIWA KUPITIA UPYA RIBA ZAO


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini zipitie
upya riba zake ili Watanzania waweze kukopa na kurejesha kwa
urahisi.

Amesema riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma
zisizokidhi mahitaji na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni
miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi
wanapotaka huduma za kifedha.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 15, 2016)
wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki
za Wananchi (COBAT) mjini Dodoma.

Mkutano huo ulijumuisha wajumbe kutoka mikoa 10 ya Kigoma,
Lindi, Simiyu, Manyara, Katavi, Mbeya, Mwanza, Morogoro,
Singida na Dodoma kati ya mikoa 18 ya Tanzania Bara ambayo
bado haina Benki za Wananchi ila ipo katika hatua za kuanzisha.

Amesema changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa
mbalimbali za sheria na taratibu ambazo zinakwamisha ufanisi
wa kiutendaji kwa baadhi ya taasisi hasa zile zinazolenga
kuwahudumia watu wa kipato cha chini.

“Tunahitaji kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi, na
Benki za Wananchi ni kiungo muhimu katika kushughulikia
changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za kifedha,”
amesema.

Waziri Mkuu amesema ni muhimu kuanzisha Benki za Wananchi
katika kila Mkoa ili kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi
na walengwa, hali ambayo itasaidia kupunguza umasikini kupitia
ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa
ambayo itaonyesha ari zaidi ya kuanzisha benki zao na akatoa
wito waandae mikakati ya kuhamasisha wananchi ili wakusanye
mitaji ya kutosha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa COBAT, Bibi Elizabeth
Makwabe amesema Jumuiya yao ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa
na wanachama saba na sasa hivi wamefikia 10 huku wananchi
wanaowahudumiwa na benki hizo ni zaidi ya milioni mbili.

Amesema Jumuiya za Benki ya Wananchi inakabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo mfumo hafifu wa Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ufinyu wa
mitaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, JUNI 15, 2016.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post