Ticker

6/recent/ticker-posts

Dkt Mwanjelwa kuzuru China kwa lengo la kuboresha mashirikiano kati ya Serikali ya China na Tanzania

Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiwa na mgeni wake Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu mara baada ya kumpokea mgeni wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiwa na mgeni wake Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo ya China, Dkt. Qu Dongyu wakiwa katika mazungumzo katika Hotel ya Serena, Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki
Waziri wa Kilimo wa Tanzania Dkt. Charles Tizeba na Naibu Waziri, Dkt. Mary Mwanjelwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Thomas Kashilila wawakimsikiliza Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu
Naibu Waziri wa Kilimo kutoka China, Dkt. Qu Dongyu akieleza namna China itakavyoendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali kulia na kushoto kwake ni Maafisa wa Ubalozi wa China nchini
Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akimkabidhi zawadi ya korosho za Tanzania Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam, jana jioni
Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa akimkabidhi zawadi ya picha yenye kuonyesha upekee wa maliasili za Tanzania, Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam, jana jioni

Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa anataraji kuzuru China mapema mwezi Mei ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya kuboresha mashirikiano kati ya Serikali hizo mbili yenye lengo la kuleta mapinduzi ya kweli kwenye Sekta ya Kilimo hususani kwenye masoko ya bidhaa za kilimo za Tanzania pamoja na eneo la kuwajengea uwezo Wakulima na Wataalamu wa Kilimo wa Tanzania.

Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba ameyasema hayo mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo katika yake na mgeni wake Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Dkt.Tizeba amesema China imeihakikishia Tanzania kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya kilimo nchini kwa kuendelea kununua bidhaa za chakula za Tanzania ambazo ni pamoja na muhogo, nyuzi za pamba, kahawa, korosho na mbegu za mafuta.

Waziri Tizeba amesema China itaendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika eneo la utaalamu kwa kupitia programu maalumu ya kusomesha Wataalamu wa kilimo nchini lakini pia kusaidia vifaa vya kitaalamu katika eneo la utafiti na mafunzo kupitia Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine na Kituo cha Cholima Dakawa vyote vya Mkoani Morogoro.

Waziri Tizeba ameongeza kuwa mara baada ya majadiliano hayo, timu ya Wataalamu imeundwa kutoka China na Tanzania ili kupitia maeneo ya kipaumbele kama walivyokubaliana na kwamba timu ya Wataalamu ya Tanzania ikiongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa itatembelea China mapema mwezi Mei kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu mashirikiano hayo na baada ya hapo Serikali zote mbili zitasaini hati za makubaliano.

“Napenda kuwafahamisha Watanzania habari njema ya zao la muhogo kupewa kipaumbele na kuundiwa timu ya kimkakati na zaidi ya yote, Ndugu zetu Wachina wameonyesha nia ya kuisaidia Programu yetu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ASDP II ambayo tutaizindua hivi karibuni” Amekaririwa Dkt, Tizeba.

Awali akizungumza mara baada ya mapokezi hayo katika uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa alimuhakikishia Naibu Waziri wa Kilimo wa China, Dkt. Qu Dongyu kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli itaendeleza ushirikiano na serikali ya china ili kuongeza kasi na uwajibikaji na kuwa chachu ya maendeleo kwa watanzania.

IMETOLEWA NA:

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA KILIMO 
ALHAMISI, JANUARI, 2018.

Post a Comment

0 Comments