Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
akizungumza Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Mtukufu Sheikh Saud Bin Saqr Al
Qasimi na kufanya nae mazungumzo yaliolenga kuendeleza uhusiano na
ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo.
Mazungumzo
hayo yaliofanyika katika makaazi ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi
mjini Ras-Al-Khaimah, ambapo viongozi hao kwa pamoja walieleza haja ya
kuendeleza uhusiano na kuimarisha mashirikiano katika kuinua sekta za
maendeleo ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia.
Aidha,
viongozi hao walizungumza juu ya hatua zinazoendelea katika suala zima
la utafiti wa mafuta na gesi asilia ambapo katika mazungumzo hayo
walieleza haja ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pamoja ili kufikia
lengo la kuipaisha Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.
Katika
maelezo yake, Dk. Shein alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na
juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kumpongeza kiongozi
huyo kwa mafanikio yaliopatikana nchini humo katika kipindi kifupi.
Rais
Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza
kutoka kwa ndugu zao wa Ras Al Khaimah na iko tayari kupanua wigo wa
maendeleo kutoka nchini humo kwani inatambua mafanikio yaliopatikana
kutokana na mikakati iliyowekwa.
Pamoja
na hayo, viongozi hao kwa pamoja walizungumzia hatua zaidi
zinazohitajika katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ras Al
Khaimah katika sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupanga mipango
madhubuti katika malengo yaliokusudiwa ya hapo baadae.
Nae
Kiongozi huyo alieleza kuwa Ras Al Khaimah itaendeleza uhusiano na
ushirikiano wake na Zanzibar hasa katika sekta hizo za maendeleo na
kusisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaletea maendeleo makubwa
Zanzibar hasa kwa kutambua kuwa jambo hilo limo kwenye dhati ya moyo
wake.
Alieleza
kuwa uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria uliopo una malengo ya
kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo endelevu huku
akizipongeza juhudi na kasi za Rais Dk. Shein za kuhakikisha Zanzibar
inapiga hatua za kiuchumi.
Katika
maelezo yake Mtawala wa Ras Al Khaimah alimuhakikishia Rais Dk. Shein
kuwa atandelea kumuunga mkono ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na umasikini na
kukuza uchumi yanatekelezeka kwa vitendo kwani kuna kila dalili za
kuyatekeleza kutokana na juhudi anazoziona ambazo zinafanywa na Dk.
Shein pamoja na Serikali anayoiongoza.
Wakati
huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya
Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya Ras Al Khaimah “Rak
Gas”, iliyopo mjini Ras Al Khaimah ambapo katika maelezo ya uongozi wa
Kampuni hiyo walimueleza Dk. Shein hatua zilizofikiwa za utafiti wa
mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Nae
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Utafiti na Uchimbaji wa
Mafuta na Gesi Asilia Kamal Ataya alimpongeza Dk. Shein kwa ziara yake
hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo huku akisisitiza kuwa
Kampuni yake itahakikisha utafiti unaofanyika unakuja na majibu mazuri.
Dk.
Shein kwa upande wake alitoa pongezi zake kwa Mtawala wa Ras Al Khaimah
pamoja na kuipongeza Kampuni hiyo kwa jitihada zake inazochukua katika
kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa na hatimae kuleta tija.
Mapema,
Rais Dk. Shein akiwa na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein,
walitembelea eneo la Kisiwa cha Al Marjan ambacho kimetengezwa baada ya
kufukiwa kwa bahari na kuwa mji wa kisasa wa kitalii na uwekezaji.
Akiwa
katika eneo hilo, Dk. Shein alipata maelezo juu ya hatua zilizochukuliwa
katika kulitengeneza eneo hilo la bahari na sasa kuwa ardhi iliyojengwa
hoteli za kisasa ambazo zimekuwa ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka
sehemu mbali mbali duniani.
Aidha,
uongozi wa Kisiwa hicho ulimueleza Rais Dk. Shein hatua zilizochukuliwa
katika kuhakikisha hata watalii wakiwemo wananchi wa Ras Al Khaimah
wanapata fursa ya kutalii katika eneo hilo kwa kuweka viwango vya chini
vya malipo ya hoteli hizo ili kuhakikisha wenye vipato vya chini nao
wanafaidika.
Dk.
Shein akiwa nchini Dubai pia, alipata fursa ya kukutana na ujumbe wa
Utaratibu wa Mfuko unaojulikana kwa jina la “Khalifa Fund” ambapo
uongozi wa Mfuko huo ulimueleza Rais Dk. Shein namna unavyotoa fursa
zake na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Zanzibar hasa katika mpango wa
kuwawezesha vijana kujikomboa na ajira na kuahidi miongoni mwa nchi
zitakazowapa kipaumbele Zanzibar itakuwa ni ya mwanzo.
Rais
Dk. Shein amemaliza ziara yake ya wiki moja katika nchi za Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE) na anatarajiwa kurejea nchini kesho Jumamosi,
tarehe 27 Januari, 2018.
Ziara
hiyo ya Dk. Shein ilianza kwa kufanya mazungumzo na Mtukufu Sheikh
Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu
Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya (UAE) nchini Abu Dhabi ambapo
pia,alifanya mazungumzo na Mohamed Saif Suwaid, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko
wa Maendeleo ya Abudhabi “Abudhabi Fund for Development”, na kutembelea
mji wa Nishati, Masdar, msikiti wa Shaikh Zayed pamoja na sehemu ya
kihistoria ya Wahat Al Karama.
Aidha,
Dk. Shein alifanya ziara nchini Dubai kufanya mazungumzo na Mtukufu
Sheikh Mohammed bin Rashid Al Makhtoum, Makamo wa Rais na Waziri Mkuu wa
(UAE) na Mtawala wa Dubai, alitembelea Bandari ya Jebel Ali, alikutana
na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wenyeviwanda wa Dubai na
kutembelea Mji mpya wa kisasa wa Nakheel pamoja na Mradi wa Palm
Jumeirah.
Dk.
Shein alifanya ziara mjini Sharjah na kukutana pamoja na kufanya
mazungumzo na Mtukufu Dk. Shaikh Sultan Mohammed Al Qasimi, Mtawala wa
Sharjah,akiwa Sharjah, alitembelea eneo la shughuli za uvuvi la ‘East
Fishing Processing LLC” pamoja na shamba la ngombe wa maziwa la Al
Rawabi.
Pia,
Dk. Shein alifanya ziara Ras Al Khaimah na kukutana pamoja na kufanya
mazungumzo na Mtukufu Shaikh Saud Saqr Al Qasimi, Mtawala wa Ras Al
Khaimah pamoja na kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Kimataifa ya
Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia ya Ras Al Khaimah “Rak
Gas” pamoja na kutembelea kisiwa cha Al Marjan.
Katika
ziara hiyo, Dk. Shein alifuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mkewe
Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira
Salama Aboud Talib, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum
Mohamed, Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalum Juma Ali Khatib,pamoja na
Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji
Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine
ni Katibu Mkuu Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Juma Ali Juma,
Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum
Khamis Nassor pamoja na watendaji wengine wa Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk