Na Hamza Temba-Dar es Salaam
...................................................................................
SERIKALI kupitia
wizara zake nne tofauti imedhamiria kukabiliana na changamoto mbalimbali za
utoaji wa huduma kwa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K. Nyerere (JNIA) jijijini Dar es Salaam.
Changamoto hizo
ni pamoja na msongamano na joto katika eneo la kuchukulia mizigo, muda mrefu wa
upatikanaji wa hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na
changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani hapo.
Mawaziri wa
Wizara hizo ambao wamefanya ziara ya pamoja katika uwanja huo jana na kukagua
shughuli za utoaji huduma ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk.Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje Dk.Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano,
Mhandisi Atashasta Nditiye.
Akizungumza
uwanjani hapo, Dk. Kigwangalla alisema wamefikia hatua ya kukutana mawaziri hao
baada ya wageni hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika kuwa wanatumia muda
mwingi kuhudumiwa katika eneo la uwanja huo kiasi cha kuwapotezea muda.
Dk.Kigwangala
amesema kutokana na malalamiko hayo ya muda mrefu na mengine kadhaa hatua
mbalimbali zimechukuliwa tangu Agosti 8 mwaka 2017 manaibu waziri wa wizara
hizo nne walipofanya ziara uwanjani hapo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi
changamoto hizo na kwamba kukutana kwao jana ni muelendezo wa kushughulikia
kero hizo ambapo mafanikio yameanza kuonekana.
Dk.Kigwangala
amesema ipo haja ya kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika viwanja vya
ndege nchini ukiwamo JNIA huku akisisitiza umuhimu wa watendaji na watoa huduma
katika nafasi mbalimbali kuwa wakarimu kwa wageni.
Amesema ni vema
hata Polisi walioko uwanjani hapo wakimkamata mgeni basi badala ya kutumia
nguvu wawe na ukarimu kwani ni muhimu kumdhibiti mgeni bila kutumia nguvu ili
ikibainika hana kosa aachiwe na asiwe na malalamiko ya kunyanyaswa.
Dk.Kigwangala
amesema kuna haja kwa wageni wanapokuja Tanzania wakirudi makwao wasimulie
ukarimu na uzuri wa nchini yetu.
Ameongeza
anatamani kuona kuanzia uwanjani hapo hadi hotelini ambako mgeni anakwenda
anatumia muda mchache, anapata nafasi ya kuona picha za viongozi mbalimbali
ambazo zitakuwa uwanjani, picha za wanyama na video ambazo zinaonesha utalii wa
Tanzania.
Amesema kumpokea
mgeni jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo muhimu
zaidi na akafafanua hata teksi ambayo mgeni ataitumia kusafiri dereva awe na
ukarimu hata wa kumsalimia na wakati mwingine kutabasamu.
Kwa upande wake,
Waziri wa Mambo ya ndani Ndani Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza baada ya ziara
hiyo alisema jitihada mbalimbali zinafanywa kutatua changamoto hizo.
Ametaja hatua
ambazo wizara yake inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati za kusafiria
kwa njia ya kieletroniki.
Pia wameamua
kuongeza idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni ikiwa sambamba na
kuongeza watoaji huduma ili kurahisisha utoaji huduma wa muda mfupi.
“Taarifa
zinaonesha kuwa kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa
tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka
hadi saa moja, lengo letu ni kushuka zaidi.
“Mbali ya
kuboresha huduma tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja
vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu.
“Tunafahamu
mataifa mengi yameitikia mwito wa uwekezaji nchini hasa katika mikakati ya
kufikia Serikali ya Viwanda na uchumi wa kati.
“Hivyo wageni
wanakuja kwa nia njema ya kuwekeza lakini hatutaki wale wenye nia mbaya kutumia
mwanya huo.Hivyo tutaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika viwanja
vyetu,”amesema.
Kwa upande wa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Dk. Susan Kolimba amesema wanaridhishwa na hatua ambazo
zinachukuliwa katika kuondoa changamoto zinazoelezwa kuwapo uwanjani hapo.
Amesema wizara
yao inatamani kuona idadi ya wageni inaongezeka zaidi na wakati huo huo
wakifurahia huduma ambazo wanazipata wakifika nchini kwetu. Alisema Wizara yake
itaendelea kuitangaza Tanzania na vitutio vyake ili idadi ya watalii iweze
kuongezeka.
“Tumefanya ziara
na binafsi niseme tu nimeridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa katika kuondoa
changamoto hizo,”amesema Dk.Kolimba.
Naye, Naibu
Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wizara yao
tayari imechukua hatua mbalimbali za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya
kufunga viyoyozi (AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.
“AC zilizopo ni
za muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja huo yalipojengwa. Hivyo
tayari zimeanza kufungwa AC mpya na ndio maana joto limepungua” amesema.
Pia amesema
wamepata kampuni ambayo itakayofanya ukarabati kwa kuongeza eneo la kukaa
wageni wanaosubiri huduma mbalimbali kabla ya kutoka uwanjani.
Amesema kuna
jitihada mbalimbali Serikali inafanya jitihada za kuondoa msongamano wa wageni
ikiwamo ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la Terminal
III ambalo litahudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa ambalo wakati
linajengwa lengo lake lilikuwa kuhudumia watu milioni moja.
“Ujenzi wa jengo
jipya umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa asilimia 100
litaanza kutumika kwa kuwa kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,’amesema.
Waziri wa Maliasili na
Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Dk. Mwigulu Nchemba wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto
mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa
wa Dar es Salaam JNIA jana kwa ajili ya kukabiliana nazo.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi
Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana wakati
wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni
hususan watalii wanaoingia nchini
kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine
walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa
pili kulia), Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye
(wa tatu kulia) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba (wa nne kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (wa tatu kushoto) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) .
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kulia) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Susan Kolimba jijini Dar es salaam jana wakati wa ziara ya pamoja ya kukagua Changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wageni hususan watalii wanaoingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam JNIA kwa ajili ya kukabiliana nazo. Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia).