MHE BITEKO AKIAGIZA KIWANDA CHA DANGOTE KUWEKA MKATABA WA UNUNUZI WA JASI KWA WACHIMBAJI WADOGO

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akitazama eneo la uzalishaji wa saruji katika kiwanda cha Dangote wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Mtwara,
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja uzalishaji wa kiwanda cha Dangote Ndg Hemendra G. Raithatha alipotembelea kiwanda hicho wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mtwara,
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja uzalishaji wa kiwanda cha Dangote Ndg Hemendra G. Raithatha kuhusu uzalishaji Wa saruji kiwandani hapo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, Leo 19 Januari 2018. 
Kikao cha kazi kikiendelea 

Na Mathias Canal, Mtwara

Uongozi wa Kiwanda cha uzalishaji wa saruji cha (DANGOTE CEMENT LTD) Mkoani Mtwara umeagizwa kuandaa  mikataba ya ununuzi wa jasi (Gypsum) na wachimbaji wadogo ili kuboresha Biashara ya wachimbaji hao sambamba na faida kwa kiwanda hicho kuliko ilivyo sasa ambapo kiwanda kinanunua Madini kutoka kwa wachimbaji wadogo bila kuwepo makubaliano maalumu yanayofanana kwa wote.

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ametoa agizo hilo leo 19 Januari 2018 wakati akizungumza na uongozi wa kiwanda cha Dangote muda mfupi baada ya kutembelea kiwanda hicho akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara.

Mhe Biteko alisema kuwa rasmi mikataba hiyo inapaswa kukamilika katika kipindi cha Siku 14 (Wiki mbili) kuanzia Leo 19 Januari 2018 hadi 2 Februari 2018  na kuwasilishwa kwenye ofisi ya madini kanda ambayo itawaita wadau wote kujadiliana vipengele vya mikataba hiyo ambayo itawafanya wachimbaji kuwa na bei ya pamoja na kutoa wajibu na haki kwa pande zote mbili.

Alisema kuwa katika mkataba huo ni lazima kuwepo kipengele cha kuwalipa ndani ya siku 30 wachimbaji Mara baada ya kiwanda kukusanya bidhaa zao jambo ambalo litaibua ufanisi na tija katika ukuzaji wa Biashara zao na kuaminika katika jamii.

Mhe Biteko alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli inataka wawekezaji wafanye kazi kwa amani pasina kusumbuliwa huku kwa upande wa wananchi wakisalia kunufaika na uwepo wa wawekezaji hao.

Alisema kuwa moja ya ajenda muhimu kwa serikali ni pamoja na kufanikisha ukuaji wa wachimbaji wadogo kufikia kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa hivyo ni lazima kuimarisha soko la ndani kwani wachimbaji wadogo hawawezi kukua kama soko la ndani halitaboreshwa.

Awali wachimbaji wa Jasi, walitoa kilio chao kwa Naibu Waziri huyo kuwa kiwanda cha Dangote hakinunui Madini yao na hata kikinunua malipo huchukua muda mrefu sana hadi miezi minne na kwamba kiwanda kinawagawa wachimbaji hao na kununua bei tofautitofauti kwa bidhaa moja jambo ambalo linawafanya wachimbaji wa Jasi kuambulia hasara. 

Aidha, Naibu Waziri wa Madini Mhe Biteko amewataka watanzania wote wanaofanya kazi kwenye migodi na kwingineko kuwa waaminifu mahali pa kazi kwani kumekuwa na malalamiko ya wizi hususani migodini jambo ambalo linapunguza imani kwa wawekezaji.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post