KAMPUNI YA PREMIUM AGRO CHEM LTD YAVUKA MALENGO KWA KUSAMBAZA TANI 19,500 ZA MBOLEA NCHINI

Malori ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakiwa tayari yamepakia mbolea kutoka maghala ya Kampuni ya Premium Agro Chem Ltd Dar es Salaam jana tayari kuisafirisha kwenda vijijini kwa wakulima ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk.John Magufuli la kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati.
Mbolea ikipakiwa kwenye magari.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC), Salum Mkumba (kushoto), akizungumza na viongozi wa Kampuni ya Premium Agro Chem Limited inayosambaza mbolea alipofanya ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam kujionea zoezi la kusafirisha mbolea kwenda mikoani. Kutoka kulia ni Meneja Masoko wa kampuni hiyo,  Brijesh Barot, Mkurugenzi Mtendaji,  Sagar Shah na Oparesheni Meneja, Rhoda Mwita.
Malori yakisubiri kupakia mbolea hiyo.


Na Dotto Mwaibale 

KAMPUNI ya Mbolea ya Premium Agro Chem Limited, imeeleza kwamba katika kipindi cha miezi mitano sasa imevuka malengo ya usambzaji wa mbolea kwenye vituo vyake tisa nchini kote, kwa kusambaza zaidi ya tani 19,500 mpaka mpaka Januari sita mwaka huu.


Kampuni hiyo, ilisema ilipewa mgawo wa tani 3,500 na serikali wa kuuza mbolea hiyo kwa wakulima kwa bei elekezi, mbolea ambayo ilinunuliwa kwa utaratibu maalum uliowekwa na serikali. 

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Sargar Shah, alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea maghala yao kujionea utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli, alilolitoa juzi wakati akimwapisha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko. 

Sargar alisema wameamua kutoa taarifa kuhusu utendaji wa kazi zao, ambapo kuanzia mwezi Septemba walisambaza zaidi ya tani 1,040 ikiwa ni sawa na mifuko 22,603 yenye ujazo wa kilo 25,na Kilo 50 kwenye vituo vyao nchini kote. 

Vituo vya kampuni hiyo vinavyotumiwa kwa ajili ya usambazaji wa mbolea kwa wakulima vipo Makambako, Njombe, Iringa, Kahama, Moshi, Songea, Mbinga na Dar es Salaam. 

Aidha, Sargar alisema kwamba mwezi Oktoba, kampuni yake ilisambaza kwa mawakala zaidi ya tani 3,202 sawa na mifuko 76,030 yenye ujazo wa kilo 25 na kilo 50 kila mmoja, ambazo ziliendelea kuuzwa kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali na kusimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA). 

“Mwezi Novemba kampuni ya Premium Agro Chem Limited, ikionyesha uzalendo wa hali ya juu iliendelea kusambaza zaidi ya tani 4,250 sawa na mifuko 92,761 yenye ujazo wa kilo 25 pamoja na kilo 50,” alisema Sargar na kuongeza yote hiyo wanafanya kumuunga mkono Rais.

Aliongeza kusema kuwa mwezi Desemba, wamesambaza zaidi ya tani 8,800 kwa mawakala wao nchini kote, ikiwa ni sawa na mifuko 186,138 yenye ujazo wa kilo 25 na kilo 50, kulingana na mahitaji ya wateja na wakulima nchini. 

Sargar, alisema mwezi Januari, walianza kusambaza mbolea kwa mawakala hao mikoani na hasa katika mikoa ambayo kuna mawakala wao, ambapo jumla ya tani 2,127 zilisambazwa kwa wadau wao nchini kote mpaka kufikia Januari 06, sawa na mifuko 42,692. 

Mkurugenzi huyo alisema kwamba makubaliano na Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) ni kupakiwa na kusambaza zaidi ya tani 1000 za mbolea hiyo kwenda katika mikoa ambayo wao hawana mawakala na kurahisha upatikanaji na pia kwa bei elekezi ya serikali. 

Meneja Biashara wa Premium Agro Chem Limited, ambaye kwa sasa ndiye anayesimamia zoezi hilo,  Brijesh Barot, alisema wamejiandaa vizuri kufanya kazi hiyo mchana na usiku kwa nia ya kufikia malengo ambayo serikali imeyahitaji. 

Barot alisema kampuni hiyo tayari kuanzia mwezi Septemba, imesambaza kwa wakulima kupitia kwa mawakala wao zaidi ya tani 19,500 za mbolea ya kupandia aina ya Urea, ikiwa kwenye ujazo wa kilo 25 na kilo 50. 

Barot aliongeza kusema kwamba, kampuni yake imeendelea kusambza na kuuza kwa wakulima mbolea zaidi kwa bei elekezi, licha ya kuwa tayari walimaliza kuuza tani 3,500 zilizoagizwa na serikali na kutakiwa kuuzwa kwa bei elekezi.  

“Sisi ni watanzania, wafanyabiashara wazalendo kwa nchi hii, hatutaki kufanyakazi kwa ajili ya kutafuta faida,badala yake tunaungana na Mheshimiwa Rais Magufuli, kuisaidia jamii kwa kufanya kazi  ili kuwakomboa kiuchumi kupitia mazao watakayopata kwa kuyauza na ziada kwa matumizi ya chakula,” alisema Barot.




Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post