Naibu Waziri wa Wizara
ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akisikiliza kwa makini maelezo kuhusu
mashine zilizotolewa na wafadhili pasina kutumika kwa muda mrefu wakati
alipotembelea Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Naibu Waziri wa Wizara
ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akikagua mashine mbalimbali wakati
alipotembelea Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara
ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi
wa Chuo cha Madini Dodoma leo 15 Januari 2018.
Na Mathias Canal,
Dodoma
Uongozi wa Chuo cha
Madini Dodoma kilichopewa ithibati kamili ya kutoa mafunzo ya umahiri yaani
Competence Based Education and Training System (CBET) umetakiwa kujitathmini
ikiwemo kutatua changamoto zinazokikabili chuo hicho ndani ya wiki mbili.
Kauli hiyo imetolewa na
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka Biteko Leo 15 Januari 2018
alipotembelea chuoni hapo na kujionea hali ya ufanisi wa chuo hicho huku
akikerwa na uduni wa utunzaji wa vifaa katika chumba cha maabara ya uchenjuaji
wa madini.
Mhe Biteko alisema kuwa
pamoja na changamoto lukuki walizoainisha katika taarifa ya chuo iliyosomwa na
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndg Vincent Willium Pazzia ikiwa ni pamoja na uchache
wa bajeti, uhaba wa wakufunzi katika fani za uhandisi na usimamizi wa mazingira
migodini na upungufu wa ofisi za watumishi, wanatakiwa kuwa na mikakati ya
kukabiliana nazo ndani ya wiki mbili zitakazofika ukomo mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema kuwa serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Dkt John Pombe Magufuli haitatoa fedha mahali ambapo hakuna matokeo ili ziliwe
na watu wasiokuwa na matakwa mema na Taifa.
Aliongeza kuwa katika
Wizara ya madini kumekuwa na malalmiko mengi kuliko utendaji jambo ambalo
lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu haraka litabakisha usugu na uvivu wa kufikiri
kwa baadhi ya watendaji na kusalia kufanya kazi kwa mazoea pasina kuwa na
ubunifu.
Naibu Waziri wa Madini
Mhe Biteko alisema kuwa wakati Taifa likiwa linaelekea kuwa katika uchumi wa
kati na mapinduzi ya viwanda huku rasilimali za madini zikipewa umuhimu mkubwa
ni lazima watendaji wakubali kukabiliana na changamoto mbalimbali kwani tiba ya
changamoto hizo ni pamoja na kuzikabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Aidha, ameutaka uongozi
wa chuo hicho cha madini kuhakikisha kuwa kinazalisha wataalamu wengi katika
sekta ya madini ambao watalisaidia Taifa kutekeleza majukumu muhimu ya serikali
ikiwemo uzalendo na ulinzi wa mali za umma.
Alisema kuwa watendaji
wote serikalini wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu kubwa moja la kuhakikisha
kuwa wanatekeleza kwa ubora na umakini mkubwa maelekezo rasmi ya serikali ambayo
yamebainishwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi
cha mwaka 2015-2020.