AFISA Ardhi wa Jiji la Arusha adaiwa kumkimbia Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangala
alipobaini anakwenda kufanyia uhakiki eneo la ekari 40 linalomilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA), ambapo kati ya hizo ekari 20 zimegaiwa kinyemela kwa wakazi 83.
Waziri Kigwangala aliwaeleza waandishi wa habari wakati akiwa kwenye eneo hilo lililopo Njiro jijini Arusha alipotembelea kujionea hali halisi kwenye kiwanja hicho namba 4081 kilichopo maeneo ya Njiro jijini Arusha akiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa NCAA! Dk Freddy Manongi.
Alisema kuwa imekuwa bahati mbaya wameshindwa kufanikisha zoezi la uhakiki baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa maafisa ardhi ambapo ameambiwa kuna afisa ardhi mmoja alifika eneo hilo lakini aliposikia kunafanyika uhakiki akakimbia na simu akazima.
"Lakini kwa sababu ni zoezi la serikali tumeona sasa tutafuata taratibu halisi za Serikali kupata maafisa ardhi ambao tutakuja kufanya nao uhakiki kesho (leo)," alisema Kigwangala ambapo ataikabidhi bodi ya Wakurugenzi ya NCAA kufuatilia suala hilo kusimamia maamuzi atakayoyatoa.
"Hata Halmashauri (jiji la Arusha) maafisa ardhi waliopo sasa wanajua eneo hilo ni la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro walipotaka uhalali kutoka kwao basi walikimbia haraka sana kusema basi tuwapeni eneo lingine kama fidia walijua kwamba walivyogawa hivi viwanja waligawa kinyemela hawakugawa kihalali," alisisitiza Waziri Kigangwala.
Alisema kuwa awali Kiwanja hicho namba 4091 kilichopo Njiro kilikuwa chini ya shirika la Utalii Tanzania, (TTC) ambapo mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati wa ubinafsishaji iliamriwa mali zote sasa Bodi ya Utalii nchini,(TTB).
Waziri Kigwangala alisema kuwa mwaka 2006 Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma,(PSRC ), walitangaza kuuza mali zilizokuwa chini ya TTB ikiwemo kiwanja hicho ambacho kilinunuliwa na NCAA kwa shilingi bilioni 1.8 ambapo kwenye eneo hilo kulikuwa na nyumba na vitu vingine lakini mpaka sasa hawakuliendeleza.
Alisemamkuwa Mwaka 2016 wakati ngorongoro wanataka kuendeleza eneo hilo kuliibuka migogoro miwili, TTB waliendelea kutambua eneo hilo kama mali yao huku eneo lingine likigawanywa na halmashauri ya manispaa ya Arusha kwa ajili ya makazi ya wananchi.
"Ikalazimika ifanyike 'official search' kwa Kamishina wa Ardhi wa kanda hii (Kaskazini) ambaye ofisi zake ziko Moshi. Ramani aliyo nayo ni ya ekari 40 na umiliki wake uko kwa jina la TTB ambalo hili liliuzwa kwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kule haitambuliki hizi ekari 20 zilizopo hapa zipo kwa makazi ya wananchi na kuwa na kuna wakazi wamegaiwa.," alisema Waziri Kigwangala na kuongeza.
Hivyo ni wazi kabisa eneo hili la hekta 10 karibu ekari 20 imegawanywa kwa matumizi ya makazi ambayo ndani yake kuna kaya 83 ambazo ziligawanywa na Halmashauri ya manispaa ya Arusha ni eneo la uvamizi.Hivyo hizi familia 83 ambazo zimevamia hapa hata kama wanahati yoyote ni hati ya kihuni ni hati isiyotambulika hivyo ni wavamizi kama wavamizi wengine tu,".
Waziri Kigwangala alidai kuwa kuna taarifa kwamba kati ya mwaka 1995 na 1996 eneo hilo la ekari 20 liligawanya kinyemela kwa hizo kaya 83 lakini walioshiriki kugawa ambapo mpaka sasa hawajathibitisha ila taarifa alizo nazo ni kwamba ni watu wa ndani wa taasisi hizohizo tatu ambazo zina mgogoro wa eneo hilo.
"Taarifa tulizo nazo ni kuwa ilitengenezwa 'syndicate' ya maafisa kutoka Bodi ya Utalii Tanzania na maafisa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lakini pia maafisa kutoka Wizara ya Ardhi. Ni taarifa ambazo hatujazithibitisha ... lakini maafisa hao walitengeneza taratibu za kihuni za kugawana eneo hilo," alisema Waziri Kigwangala huku akisisitiza kuwa muda si mrefu ukweli utajulikana.
Alisema amewasiliana na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi ambaye amemuagiza Kamishina wa Ardhi aitishe watu wote ambao wanamgogoro na eneo hilo la Serikali wapeleke nyaraka zao kwa kamishina wa ardhi zoezi linalotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
"Na sisi tutabaini ukweli kwamba hawa waliopo hapa ni kina nani manake kuna maneno yanasemwa kuna baadhi ya Mawaziri Wakuu Wastaafu wawili wanamaeneo yao, baadhi ya maafisa waliokuwepo zamani wa hifadhi ya Ngorongoro, kuna baadhi ya maafisa wa Bodi ya Utalii zamani wanayo maeneo yao hapa lakini kwa sababu hatujui majina yao hatuwezi kusema ni akina nani lakini tuna taarifa hizo," alisema Kigwangala.
Alisema kuwa watu hao majina yao yatakajulikana kwa kamishina wa ardhi watachukuliwa hatua za kisheria kwa kutumia vibaya madaraka yao na wavamizi wengine wataondolewa kwenye eneo hilo walilovamia au watatakiwa kulipa fidia.
Hata hivyo alisema kuwa wanaangalia kama wataona eneo lililobaki la ekari 20 linawatosha NCAA kwa mipango waliyojiwekea basi watakubaliana na kulipwa fidia lakini ikiwa watahitaji eneo lote la ekari 40 itawabidi kuwandoa wakazi hao na kuvunja nyumba hizo.
"Eneo hili ni 'potentia' sana ni very 'prime' kwa hapa Arusha lina 'attract' bei ya juu sana kwa mauzo kwa mimi binafsi hainishangazi kuona viongozi wa zamani wakishirikiana na maafisa wa zamani wali 'conspire' kugawana eneo hili kinyemela ni jambo la kawaida tu ambalo kwa watu wenye tamaa wanaweza kufanya," alisisitiza Waziri Kigwangala.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NCAA, Manongi alisema kuwa walipanga kujenga jengo kubwa la utalii miaka 10 iliyopita na michoro ilikuwe imeshaandaliwa ila kwa sasa itabidi warudi wakajadiliane watumie eneo hilo kwa matumizi gani.