MBUNGE RITTA KABATI ATOA MSAADA WA MAFUTA MAALUM YA KUPAKA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI MKOA WA IRINGA

Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi box la mafuta hayo katibu wa Tas mkoa wa Iringa bwana Leo Sambala katika ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa  
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi boxi  la mafuta hayo katibu wa Mufindi bwana Andrea Kihwelo
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi  mafuta hayo moja ya walemavu wa ngozi
 Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati akimkabidhi boxi la mafuta hayo mwenyekiti wa wilaya ya Kilolo ndugu Anna Masasi 


Na Fredy Mgunda,Iringa

JAMII imetakiwa kuwalea, kuwatunza na kuwajali watu wenye ulemavu wa ngozi albino kwa kuhakikisha kwamba wanaishi katika mazingira mazuri, yenye usalama na sio kuwanyanyapaa pale wanapohitaji mahitaji yao ya msingi.

Aidha Chama cha walemavu wa ngozi (TAS) mkoa wa Iringa kimeshauriwa kuendelea kushirikiana na serikali, ili walemavu hao pia waweze kupata elimu juu ya afya ya usalama wa ngozi pamoja na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili katika maisha yao.


Hayo yalisemwa na mbunge wa viti maalum Ritta Kabati wakati alipokuwa akitoa msaada wa mafuta maalum ya kupaka watu wenye ulemavu wa ngozi albino katika hafla fupi iliyohudhuriwa na walemavu hao ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa


“Nampongeza Mwenyekiti wa TAS mkao wa Iringa kwa jitihada zake alizozifanya juu ya namna ya kupata mafuta haya, kama chama endeleeni kuwa wabunifu namna ya kulisaidia kundi hili tete la walemavu kwa kuwalea na kuwatunza katika mazingira mazuri”, alisisitiza mbunge Kabati 

Vilevile Kabati  aliongeza kwa kuwataka viongozi wa chama hicho kutumia fursa waliyopewa na wanachama wao, kuhakikisha kwamba wana ainisha matatizo waliyonayo walemavu wa mkoa wa Iringa na kuyafikisha katika ofisi za serikali ili yaweze kufanyiwa kazi.

Kabati alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inahakikisha kuwa inafakiwa kutatua matatizo ya wananchi wa ikisha maisha yao yanaboreshwa.

“Hata haya mafuta yamenunuliwa na serikali kupitia wizara ya afya ,maendeleo ya jamii ,jinsia ,wazee na watoto na yanasambazwa nchi nzima hivyo sisi viongozi kazi yetu ni kwasaidia usafiri walememavu hawa” alisema Kabati


Awali akitoa maelezo mafupi juu ya changamoto zinazowakabili albino katika mkoa wa Iringa huo, Mwenyekiti wao Hellen Machibya  alisema kuwa wanashindwa kuwafikia wanachama wake kwa urahisi kutokana na kukosa usafiri na rasilimali fedha, kwa ajili ya kuwatimizia mahitaji yao ya msingi. 

Machibya alifafanua kuwa kukosekana kwa fedha kunakwamisha utendaji kazi na uendeshaji wa shughuli husika, hivyo wanaiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwa kutatua kero zinazowakabili ili kundi hilo tete liweze kusonga mbele kimaendeleo.

Machibya alisema kuwa kazi aliyoifanya mbunge huyo ni kuokoa maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuwa watakuwa wanajikinga na mionzi ya jua.

Machibya alisema kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi wamekuwaathirika wakubwa wa ugonjwa wa kasa kutokana na ngozi zao kushambuliwa na jua na kusababisha kuiathiri ngozi hivyo msaada uliotolewa na serikali umeokoa sana maisha.

“Jamani sisi watu wenye ulemavu tunapenda sana kufanya kazi tatizo mionzi ya jua inatuathiri sana na kusababisha kushindwa kufanya kazi zetu kwa uwezo wetu hivyo tunaomba serikali na wadau kama mbunge Ritta Kabati waendelee kutusaidia maana mafuta haya dukani ni gharama sana hivyo watu wenye ulemavu wa ngozi hatuzimudu” Machibya

Lakini Chama cha walemavu wa ngozi (TAS) mkoa wa Iringa wamemshukuru mbunge wa viti maalum Ritta Kabati kwa kuwasidia kuwafikishia mafuta ya kujipaka mwilini kwa ajili ya kujikinga na mionzi ya jua ambayo imekuwa ikiwasababishia kupata ugonjwa wa kansa.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post