Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Mtaa wa
Chisichili Kata ya Mkonze mkoani Dodoma wakati wa ziara yake kujionea
hali ya upatikanaji wa umeme.
Mbunge
wa Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Antony Mavunde (aliyesimama),
akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa
pili kutoka kulia), kujionea hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo
mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Naibu
Waziri wa Nishati Subira Mgalu (kulia) akibadilishana mawazo na
wananchi wa Mtaa wa Chisichili, Kata ya Mkonze mkoani Dodoma wakati wa
ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa umeme. Kulia kwake ni Mbunge
wa Dodoma Mjini Antony Mavunde.
Wananchi
wakimsikiliza Naibu Waziri Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati wa
ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo
mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Wananchi
wakiuliza maswali na kutoa maoni mbele ya Naibu Waziri Subira Mgalu
(hayupo pichani) wakati wa ziara yake kujionea hali ya upatikanaji wa
umeme katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini.
Na Veronica Simba – Dodoma
Serikali
imebainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 499 zimeidhinishwa na Bunge
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme nchini kote katika mwaka huu wa
fedha unaoendelea.
Hayo
yalisemwa jana, Januari 24 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
akiwa katika ziara katika maeneo mbalimbali ya Dodoma Mjini kwa ajili ya
kujionea hali ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu pamoja na
kuzungumza na wananchi.
Naibu
Waziri Mgalu, ambaye aliambatana na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony
Mavunde aliwaambia wananchi wa maeneo aliyotembelea kuwa, kiasi hicho
cha fedha ni kikubwa na kitawezesha utekelezaji wa miradi hiyo ya umeme
katika vijiji vyote 7873 vilivyosalia nchi nzima.
“Tunamshukuru
Mheshimiwa Rais John Magufuli pamoja na Bunge la Jamhuri kutuidhinishia
kiasi hicho cha fedha. Kazi yetu sisi wasaidizi wake katika Wizara ya
Nishati ni kuhakikisha tunatekeleza jukumu alilotutuma la kuwapelekea
wananchi kote nchini nishati ya umeme wa uhakika. Tunaahidi hilo
litafanyika kwa ukamilifu.”
Akizungumzia
umuhimu wa nishati ya umeme, Naibu Waziri alisema kuwa, sekta zote
zinategemea umeme ili zifanye kazi kwa ubora. Alitoa mfano wa sekta ya
afya ambayo pasipo umeme wa uhakika haiwezi kutoa huduma bora. “Vivyo
hivyo kwa sekta ya elimu, kilimo, viwanda na nyinginezo,” alisisitiza.
Aidha,
Naibu Waziri Mgalu alitoa maagizo kwa uongozi wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kuhakikisha Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo
wanatoa kipaumbele kwa taasisi za kijamii kama vile shule, vituo vya
afya, nyumba za ibada, miradi ya maji na nyinginezo. Hata hivyo alisema
Wakandarasi lazima wahakikishe hakuna mtu au eneo linalorukwa wakati wa
kutekeleza mradi huo.
Vilevile
aliwataka wananchi kufanya maandalizi ya kuunganishiwa umeme katika
makazi yao na katika miradi na taasisi mbalimbali. “Tunataka zoezi la
kupitisha umeme katika maeneo yenu likikamilika tu nanyi bila kuchelewa
mnaunganishiwa katika nyumba zenu, hivyo anzeni kufanya maandalizi
sasa.”
Awali,
akizungumza katika ziara hiyo, Mbunge Mavunde ambaye pia ni Naibu
Waziri kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na
Vijana, alisema kuwa wananchi wa Dodoma ni wakulima wazuri wa zabibu na
mazao mengine mbalimbali, hivyo wanahitaji huduma ya umeme wa uhakika
ili kuboresha kazi zao za kilimo kwa kuanzisha viwanda vya usindikaji
ili kuongeza thamani.
Meneja
wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zakayo Temu alisema zoezi la
kufanya tathmini ya awali kwa ajili ya kutekeleza Mradi huo katika
maeneo yaliyosalia litaanza mapema mwezi Februari mwaka huu.
Ziara ya Naibu Waziri Mgalu ilihusisha Kata za Mpunguzi, Matumbulu, Mkonze, Nala na Ipagala zilizopo Dodoma Mjini.