FURSA NYINGINE YA SCHOLARSHIP YAJA: SHULE ZA SEKONDARI ZATAKIWA KUTUMA MAOMBI SASA KUSHIRIKI MAONYESHO YA SAYANSI YA YST 2018!




 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila akikabidhi zawadi kwa Prosper Gasper na Erick Simon kutoka Shule ya Sekondari St. Jude's jijini Arusha baada ya kuibuka washindi wa jumla wa Mashindano ya Wanasayansi Chipukizi (YST) yaliyofanyika leo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
SHULE za Sekondari nchini Tanzania zimetakiwa kuanza kutuma maombi sasa ili kupata fursa ya kushiriki katika Maonyesho ya 8 ya Sayansi kwa wanafunzi yanayoandaliwa na Shirika la Young Scientists Tanzania (YST) kila mwaka.
Taarifa kutoka YST zimeeleza kwamba, maonyesho hayo ni kwa wanafunzi wa kuanzia kidato za kwanza hadi cha sita kwa shule zote za sekondari – za umma na binafsi – zilizoko nchini.

“Mwisho wa kutuma maombi ni Machi 31, 2018 na maonyesho hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam mwezi Agosti,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, kutuma mapema maombi kutasaidia hata zoezi la mchujo ili kuwapata washiriki wenye mawazo yatakayoleta ushindani pamoja na ubunifu kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini Tanzania.
Jumla ya mawazo 100 yanatarajiwa kushindanishwa mwaka huu ambapo washindi katika vitengo mbalimbali watapatiwa zawadi za fedha pamoja na ufadhili wa masomo ya chuo kikuu.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, wanafunzi Prosper Gasper na Erick Simon wa shule ya Sekondari ya St. Jude’s kutoka Arusha, ndio walioibuka mabingwa wa jumla wa sayansi katika Maonyesho ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania 2017 kutokana na wazo lao la “Kutumia Simu za Mkononi kama Mfumo wa Kubaini Ajali za Moto” (The Use of Mobile Network as a Fire Alert System).
Kwa ushindi huo, mbali ya kutunukiwa medali na tuzo, pia walipata kitita cha Shs. 1,800,000 pamoja na udhamini wa masomo yao hadi elimu ya juu.
Aidha, walipata nafasi kwa mara ya kwanza ya kushiriki mashindano ya ubunifu wa sayansi na teknolojia yaliyofanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini mwezi Oktoba 2017 na mwaka huu 2018 watashiriki maonyesho ya kimataifa ya sayansi na teknolojia jijini Dublin, Ireland.
Kumekuwepo na ongezeko kubwa la ushiriki wa shule za sekondari kutoka shule 4 mwaka 2011 hadi 100, hatua ambayo imetokana na hamasa ya kuendeleza masomo ya sayansi kwa shule mbalimbali za sekondari nchini.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, uwepo wa maonyesho hayo ya sayansi kwa wanafunzi usaidia ufaulu wa masomo ya sayansi kwa shule nyingi za sekondari nchini, mfano mmojawapo ukiwa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2017, kwa mara ya kwanza shule hiyo ilipata daraja kwa kwanza (Division One) kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi, jambo ambalo lilikuwa adimu.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini umebaini kwamba, kwa miaka takriban 10 mchepuo wa masomo ya sayansi, Kemia, Baolojia na Jiografia (CBG), haujawahi kutoa hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la kwanza katika matokeo ya kidato cha sita.
MaendeleoVijijini imegundua kwamba, miaka yote ufaulu mkubwa wa masomo ya sayansi shuleni hapo umekuwa daraja la pili (division two) ambao nao haukuwa wa kuridhisha ikilinganishwa na masomo ya sanaa na uchumi, huku wanaochukua mchepuo wa sayansi ‘wakiongoza’ kwa kupata daraja la nne pamoja na kupata sufuri.

Kati ya wanafunzi nane waliopata Daraja la Kwanza mwaka 2017 shuleni hapo, wawili walikuwa wanachukua mchepuo wa sayansi na kati ya wanafunzi 57 waliopata daraja la pili, 17 wanatoka mchepuo wa sayansi pia.
Wanafunzi wawili waliopata daraja la pili shuleni hapo Diana Sosoka na Nadhra Mresa, ambao walikuwa washindi wa jumla mwaka 2016 katika maonyesho hayo ya sayansi ya YST nao walionyesha kushangazwa na matokeo hayo.
“Kweli ni maajabu kwa mara ya kwanza kuna Division One kwenye CBG pale shuleni kwetu, ni mafanikio ambayo yametokana na hamasa ya kuwepo kwa mashindano haya ya sayansi na sisi tunashukuru kuwa sehemu ya mafanikio,” anasema Diana.
Diana na Nadhra ambao walipata ushindi kwa kubuni mashine ya kienyeji ya kutotoresha mayai, pia walipata udhamini wa masomo ya chuo kikuu kutoka taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.
Wote kwa pamoja walikuwa wanachukua mchepuo wa Kemia, Baolojia na Jiographia (CBG) na kwa bahati nzuri, wote wawili wamepata Division Two ya alama 12.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post