BREAKING NEWS

Wednesday, July 27, 2011

AHAIDI KUTOA KOMPYUTA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI ZA JIMBONI KWAKE

MBUNGE wa Jimbo la Babati Vijijini mkoani Manyara Virajlal Jituson ameahidi kusambaza kompyuta katika shule zote 31 za sekondari zilizopo jimboni kwake kwa ajili ya kufikisha elimu ya mawasiliano kwa njia ya mtandao kwa wanafunzi wa shule hizo.




Jituson alitoa ahadi hiyo kwenye mkutano wake na wananchi wa mji mdogo wa Magugu,ambapo alikuwa katika ziara ya kuwatembelea na kuwashukuru wakazi wa jimbo lake kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa mbunge wao.




Alisema kutokana na hali ya sasa dunia kuwa kama kijiji,amelenga kutoa kompyuta kwa shule hizo ili kuwawezesha wanafunzi wa shule hizo wajifunze kwa kwenda na wakati katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.



Mbunge huyo pia alisema amekipatia kituo cha afya cha Magugu,kitanda maalum kwa ajili ya kuwaweka watoto wanaozaliwa kabla ya kufikisha miezi tisa (njiti) kwani huduma hiyo ilikuwa inapatikana mbali,katika hospitali ya Dareda.




“Pamoja na hayo ndugu zangu mnatakiwa muwe makini na gonjwa la ukimwi kwa kuepuka na uasherati kutokana na wafanyabiashara mbalimbali wanaokuja hapa Magugu kwa ajili ya kununua mchele,” alisema Jituson.




Pia Jituson aliwashauri wakazi hao kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji hasa katika msimu huu wa uhaba wa chakula,ili kujiongezea chakula kitakachowakutanisha na msimu ujao wakati huu wa uhaba wa chakula.




Alisema kata ya Magugu inasifika kwa kilimo cha mpunga unaozalisha mchele bora,hivyo wakazi hao wawe makini kwenye uuzaji wa mazao yao kuliko kukimbilia kuuza kisha baadaye familia zao zina angaika kwa kukosa chakula.




“Ndugu zangu wananchi wa Magugu tutumieni vizuri miradi yetu ya kilimo cha umwagiliaji ili tulime mazao ya aina mbalimbali tuweze kujipatia fedha za kutosha zitakazokidhi mahitaji yetu,” alisema Jituson.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates