BREAKING NEWS

Monday, July 18, 2011

ROLLING YATOA VIJANA WENGI



Mkurugenzi wa Rolling stone Ally Mtumwa akiongea na waandishi wa habari



MASHINDANO ya soka ya vijana ya Rolling Stone yalianza mwaka 2000 wakati huo yakishirikisha timu za mkoa wa Arusha kabla ya kupanuka taratibu na hadi sasa kuwa ya kimataifa.



Hadi kufikia hatua ya sasa ya kushirikisha timu kutoka nje ya Arusha na hadi zile za nchi za jirani, kituo cha Rolling Stone kinachoandaa mashindano hayo kimepitia katika hatua kibao ngumu.



Mara nyingi mafanikio hayaji kama mvua ila kwa jitihada kubwa kutoka kwa wale wenye moyo na nia ya kuona kitu Fulani kina songa mbele, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa viongozi wa Rolling Stone, ambao usiku kucha hawakulala wakifikiria jinsi ya kuliendeleza soka ka Bongo.



FAIDA:

Mashindano hayo yamekuwa faida kubwa kwa wachezaji wa hapa nchini na hata wale wanaokuja na timu zao kutoka nje, kwani yamewasaidia sana kukuwa kwa vipaji vyao na kuonekana na hatimaye kupaya soko ndani na nje ya nchi.



Mkurugenzi wa kituo hicho cha kusaka na kukuza vipaji vya watoto cha Rolling Stone, Ally Mtumwa akitolea mfano baadhi ya faida wazipatazo vijana alisema kuna baadhi ya wachezaji wa Tanzania wamepata timu nje ya nchi.



Alisema kuwa mbali na timu hizo za nje ya nchi, pia kuna wengi wamepata timu kubwa za hapa nchini ambazo zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na wengine sasa wamekuwanyotakatika klabu na hata taifa.



Kituo chao kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 12, 15 na hata 20, ambao ni rika linalofundishika na kuwafanya kuwa na msingi imara katika soka wanapokuwa wakubwa.



WACHEZAJI:

Mtumwa anasema kuwa taasisi hiyo ina kila la kujivunia baada ya kutoa wachezaji wanaotamba katika soka kwa sasa hapa nchini, ambao aliwataja baadhi yao kama akina Erasto Nyoni, Amiri Mftah, Nurdin Bakari, Yahaya Tumbo, Kigi Mkassy pamoja na Hafisi Mussa, ambaye kwa sasa anaichezea timu ya taifa ya Burundi baada ya kupewa uraia wan chi hiyo.



Baadhi ya wachezaji waliopitiakatika kituo hicho kwa sasa wako katika timumbalimbali kubwa na wengine wamewahi au wanaendelea kuichezea timu za taifa za Tanzania .



Mfano katika timu ya vijana ya Serengeti Boys kuna baadhi ya vijana waliowahi kuichezea timu hiyo ambao walipitia katika kituo cha Rolling Stone ni pamoja na akina David Mwantobe, Mwidini Bakari, Amiri Maftah na wengineo wengi.



MASHINDANO:

Mtumwa anasema kuwa lengo kuu la kuanzisha kituo hicho ni kuibua na kukuza vipaji vya watoto na kuwashirikisha katika mashindano, ambayo yatakuwa kama kipimo cha uwezo au kiwango chao.



Amesema kuwa baada ya kuyaanzisha mashindanohayo mwaka 2000 na kuanza na timu za jijini Arusha, baadae yaliendelea kukua na mwaka uliofuata, yaani 2001, walipata timu kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga pamoja na Kilimanjaro.



Kadri miaka ilivyozidi kwenda timu zilizidi kupata muamukoa na kuongezeka kuwa nyingi na ilipofika mwaka 2003 timu za nje ya nchi ziliweza kujiunga na mashindano haya, ambapo timu kutoka nchi za Kenya na Uganda , zilijiunga na mashindano hayo.



Mwaka 2004, mashindano hayo yalizidi kuimarika na kuwa bora zaidi kiasi cha kushirikisha na timu kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambazo zilijiunga na timu zingine za Afrika Mashariki.



Mashindano haya ya Rolling Stone yanachezwa kwa mfumo wa Ligi, ambapo timu zimegawanyika katika makundi manne ya ABCD.



Timu zilizopo katika kundi A ni Jamhuri kutoka mkoani Arusha, Simba Sport Club ya jijini Dar es Salam, Coast Union ya Tanga, Toto African pamoja na timu ya Mbaspo kutoka mkoani Mwanza pia.



Kundi B linaundwa na timu za Nyota kutoka mkoani Arusha, Saadan kutoka mkoani Pwani, Rolling Stone ambayo ndio wenyeji wa mashindano hayo na Bishop Dunning za Arusha.





Kundi C lina timu za Ruvu Shooting kutoka Pwani, Street Talent kutoka mkoani Mwanza,Young Salimbe kutoka nchini Kenya pamoja na Flamingo kutoka mkoani Arusha.



Kundi D lina timu za JKT Oljoro ya Arusha, TSC ya mkoani Mwanza, Azam ya mkoani Dar es Salaam , Cipt kutoka mkoani Arusha pamoja na timu ya vijana kutoka nchini Burundi .



WADHAMINI:

Wakati umefika sasa kwa wadhamini kujitokeza kusaidia vituo kama Rolling Stone na vingine, ambavyo vimekuwa vikijitahidi kukuza na kuuendelea mchezo wa soka hapa nchini.



Mfano kampuni inapojitokeza kuidhamini timu ya soka ya taifa ya wakubwa, ijaribu pia kuzidhamini timu za taifa za vijana, kwani msingi wa soka unaanzia kwa vijana.



Katika nchi nyingi mfano Nigeria , Ghana , Cameroon , Misri na hata Ethiopia , kampuni inayodhamini timu ya taifa ya wakubwa, ndio imekuwa ikizidhamini timu za vijana kwa kutoa huduma muhimu ikiwemo jezi na hata mahitaji mengine muhimu.



Serikali pamoja na kutozisaidia timu za taifa moja kwa moja, iweke sera nzuri ambazo zitawafanya wadhamini kujitokeza kwa wingi kuzisaidia timu hizo pamoja na vituo vinavyolea wachezaji chipukizi kama kile cha Rolling Stone.



Sera hiyo pia itazame kwa kina baadhi ya vituo ambavyo vimekuwa na ubabaishaji mkubwa, ambapo badala ya kuendeleza michezo ukiwemo soka, vyenyewe vinatafuna pesa za wahisani kupitia mgongo wa kuendeleza vipaji vya watoto wakati sio kweli.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates