BREAKING NEWS

Saturday, July 2, 2011

MGOGORO WA ARIDHI WAZUKA SIMANJIRO

MGOGORO mkubwa wa ardhi umeibuka katika kijiji cha Lormolijoi kata ya Langai wilayani Simanjiro mkoani Manyara mara baada ya baadhi wananchi wa kijiji hicho kumshutumu diwani wa kata hiyo,Lesikar Sipitek na baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji hicho kwa kugawa maeneo katika vitongoji viwili ndani ya kata yake bila ridhaa ya wananchi.

Wananchi wa kijiji hicho wamewashutumu viongozi hao kuwa wamegawa vitongoji vya Alatukuta na Lormorijoi kwa ubabe bila ridhaa ya wananchi hali ambayo imesababisha mgogoro na mpasuko ndani ya jamii yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo kwa lengo la kujua undani wa sakata hilo wananchi hao walidai kuwa tukio hilo ambalo lina histiria ndefu lilianza pale ambapo viongozi wa kijiji hicho mnamo mwaka 2007 ambapo viongozi wa kijiji hicho akiwemo diwani wao waliamua kugawa maeneo katika vitongoji vya Alatukuta na Lormorijoi bila wao kushirikishwa.

Baadhi ya wakazi hao waliojitambulisha kwa majina ya Noah Kibunda na Lucas Ngukuru waliwaambia waandishi wa habari ya kuwa pamoja na kufikisha malalamiko yao kuhusiana na vitendo hivyo kwa ngazi za serikali lakini hadi leo hawajapatiwa majibu.

Walisema kuwa kitendo kilichofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji hicho akiwemo diwani,Sipitek hakikupata Baraka yoyote kupitia mkutano wa serikali ya kijiji huku wakiiomba serikali watu waliopewa maeneo katika kitongoji cha Alatukuta warudishiwe mapema.

Hatahivyo,walibanisha ya kuwa awali walifikisha malalamiko yao kwa kumwandikia barua mkuu wa wilaya ya Simanjiro kuhusiana na malalamiko yao lakini hadi leo hawajapata majibu yoyote.

Kufuatia malalamiko hayo gazeti hili lilimtafuta diwani wa kata hiyo anayeshutumiwa(Sipitek) ambapo alipinga vikali madai ya wakazi hao huku akisema kuwa kamwe hakuhusika na mpango wa kugawa maeneo yanayotajwa bila ridhaa ya wananchi.

Sipitek,akizungumza kwa jazba alisema kuwa uongozi wake umekuwa ukifuata taratibu husika katika kuyagawa maeneo mbalimbali ndani ya kata yake huku akisisitiza kwamba madai hayo hayana ukweli kwani yana lengo la kumchafua mbele ya jamii na kutaka mkuu wa wilaya hiyo aulizwe juu ua suala hilo.

“Si kweli hao waliokueleza sisi tumefuata taratibu zote katika ugawaji wa maeneo hayo hata nyaraka zipo hao wanataka kunichafua tu,wewe ukitaka ukweli muulize na mkuu wa wilaya”alisema Sipitek

Mkuu wa wilaya hiyo,Halid Mandia alitafutwa kwa njia simu na gazeti hili hakuweza kupatikana lakini alipotafutwa mkurugenzi wa wilaya hiyo,Mohammed Nkya alijibu kwa kifupi “niko kwenye kikao nipigie baadaye”na alipotafutwa baadaye simu yake ya mkononi haikuweza kupatikana.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates