BREAKING NEWS

Wednesday, July 27, 2011

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUSHIRIKI KUPAMBANA NA RUSHWA

VIONGOZI wa dini wa madhehebu mbalimbali nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwaelimisha waumini wao madhara ya matumizi ya rushwa nchini.




Hayo yalielezwa mjini Babati na Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara (Ras) Claudio Bitegeko,kwenye mafunzo ya viongozi wa dini juu ya kudhibiti rushwa nchini,iliyoandaliwa na Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoa wa Manyara.




Bitegeko alisema hakuna shaka kwamba taasisi za dini ni wadau muhimu kwenye mapambano dhidi ya rushwa,hivyo viongozi wajenge mshikamano na ushirikiano wa tatizo la rushwa na ukiukwaji wa maadili kwa jamii hapa nchini.




Alisema viongozi wa dini wanatakiwa kuwaeleza waumini wao bila kuwaogopa kwa kuangalia cheo chake,ikiwa tajiri au masikini na waelezwe kwamba rushwa ni dhambi na Mungu hapendezwi nayo na pia ni kosa la jinai kwa sheria za nchi yetu.




“Viongozi wa dini mnatakiwa muwe mfano wa kupingwa rushwa lakini wengine mnalalamikiwa na waumini kwa ukiukwaji wa maadini kwani wengine wanalalamikiwa kwa kutoa rushwa ili wachaguliwe kuwa viongozi wa misikiti au makanisa,” alisema.




Alisema baadhi ya viongozi wa dini huwa wanatoa rushwa ili wapangiwe vituo vya mijini kwenye utoaji mkubwa wa sadaka kuliko vijijini na pia baadhi yao wanalalamikiwa kwa kuwaalika viongozi wa siasa na Serikali kwenye uzinduzi wa misikiti na makanisa na wanapokea fedha zilizopatikana kwa njia ya rushwa.




Wakizungumza kwenye mafunzo hayo baadhi ya viongozi hao wa dini walidai kuwa ni wajibu wao kuwaelimisha waumini wao na jamii iliyowazunguka madhara ya rushwa.




Walisema wataendelea kuwaelimisha waumini na jamii kwa ujumla kufuata mwenendo mwema wa maisha kwa kufanya kazi kwa bidii ili kunyanyua maisha yao,kutokata tamma na kukemea vitendo viovu ikiwemo rushwa na kujenga ujasiri wa kutoa taarifa ya watu wanaopokea rushwa.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates