BREAKING NEWS

Saturday, July 30, 2011

Flag this message MAMILIONI YATUMIKA KUJENGA WODI YA WATOTO

JUMLA ya kiasi cha sh,182,424,868,00 millioni zimetumika kukamilisha ujenzi wa wadi wa watoto katika hospitali ya Nkoaranga inayomilikiwa chini ya kanisa la kiinjili la Kilutheri (KKKT) iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Kati ya fedha hizo kiasi cha sh,12,000,000 millioni zilitumika kugharamia ujenzi wa msingi wa wadi hiyo ambao ulianza mnamo mwezi machi mwaka huu na kutambulika kama mradi wa Watoto Project uliofadhiliwa kwa msaada wa raia wa nchini Ubelgiji.

Hayo yalisemwa na mganga mkuu wa hopsitali hiyo,Dk Julis Mollel wakati wa uzinduzi wa wadi hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani humo ambapo ulihudhuria na viongozi wa kiserikali,chama pamoja na wale wa dini.

Akitoa taarifa fupi wakati wa uzinduzi wa wadi hiyo,Mollel alisema ya kuwa kukamilika kwa wadi hiyo kutasaidia kupunguza kero ya mahitaji ya watoto mbalimbali waliokuwa wakikosa nafasi katika hospitali hiyo kutokana na uhaba wa vyumba vya kuwahifadhia.

Alisema kuwa wadi hiyo yenye vyumba zaidi ya sita ambapo chumba kimoja kitakuwa kikihifadhi jumla ya watoto 20 litapunguza kero ya mahitaji ya huduma hopsitalini hapo huku akifafanua ya kuwa wadi hiyo pia itakuwa na chumba cha wagonjwa mahututi pamoja na upasuaji.

Alifafanua ya kuwa wazo la mradi huo lilitokana na daktari wa kujitolea wa nchini Ubelgiji,Tanya Van Brackel ambapo mara alipofika hospitalini hapo miaka ya nyuma walizungumza namna ya kusaidia ujenzi wa wadi wa upasuaji ambapo mara baada ya raia huyo kuona umuhimu wa hitaji hilo aliishirikisha familia yake na kuanza kuchangia mradi huo hadi kukamilika.

Naye,mkurugenzi wa mradi huo ambaye pia ni baba mzazi wa Van Brackel,Luc Van Brackel alisema kuwa amefarijika sana baada ya kukamilika kwa mradi huo kwa kuwa mara kwa mara walikuwa wakifikiria ni lini wataukamilisha.

Aliitaka jamii hapa nchini kuona umuhimu wa hitaji la kuchangia watu wenye matatizo mbalimbali hususani watoto wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali na kudai watoto hao ni tumaini na tegemeo la baadaye.

Askofu mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT) dayosisi ya Meru,Paul Akyoo aliishukuru serikali kwa kuwa bega kwa bega wakati wa muda wote wa ujenzi huo na kusema kuwa kumamilika kwa ujenzi huo kutapunguza kero kwa wakazi wa wilayani Arumeru.

Hatahivyo,akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha,afisa tarafa ya Pori wilayani humo,Senyi Ngaga alisema kuwa serikali itaendelea kushirikiana bega kwa bega na uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha inatoa huduma kwa wakazi wilayani humo ipasavyo bila vikwazo.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates