BREAKING NEWS

Wednesday, July 27, 2011

MADIWANI WATAKIWA KUTOWAKATAA WATUMISHI WAO

madiwani nchini wametakiwa kutowakataa watumishi wanaofanya kazi kwenye Halmashauri zao kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya utumishi wa umma namba nane ya mwaka 2002 na kanuni yake ya mwaka 2003.




Hayo yalielezwa na Mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoani Manyara,Anatory Choya wakati akizungumza kwenye Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kilichofanyika wilayani humo.




Choya alisema agizo hilo limetokana na waraka uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mohamed Pawaga.




Alisema waraka huo umetolewa kutokana na mtindo wa muda mrefu wa madiwani kuwakataa watumishi na kutoa adhabu kwa wakurugenzi wa halmashauri hali ambayo ni kinyume na sheria ya utumishi wa umma.




Alisema waraka huo unatambua mabaraza ya madiwani kwenye halmashauri kuwa ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wote wa halmashauri isipokuwa mkurugenzi na walimu walio chini ya mamlaka ya nidhamu ya tume ya utumishi wa umma.




Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mabaraza ya halmashauri ya wilaya nchini mara nyingi yamekuwa yakivunja sheria hizo kwa makusudi,badala ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaowatuhumu.




“Athari za ukiukwaji huu wa sheria zimetajwa kuwa ni pamoja na halmashauri husika kujiendesha kinyume na misingi ya utawala bora na pia kuonyesha uwezo mdogo wa kutekeleza sheria zake,” alisema Choya.




Alisema kutokana na makosa hayo watumishi wenye makosa huamishiwa halmashauri nyingine na kuambukiza utovu wa nidhamu,badala ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu ambazo zipo kwenye uwezo wa madiwani hao.




“Kutokana na hali hiyo mara nyingi watumishi huwa wanafanya kazi yao kwa nidhamu ya woga kwa madiwani hao badala ya kufanya utendaji wao kwa morali inayotoka mioyoni mwao,” alisema Choya.




Hata hivyo,baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walidai kuwa wataendelea kutetea maslahi ya watu wa jimbo la Mbulu na hawatakubali kuendelea kufanya kazi na mtumishi wa halmashauri hiyo ambaye hatakuwa na uchungu na maendeleo ya Mbulu.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates