Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akielezea dhamira ya kuanzishwa kwa Ikungi Half Marathon ofisini kwake
Na Mathias Canal, Singida
Ni kama vile kuwa na kiu kizito kinachohitaji maji ya kunywa na kisha
maji yakakutikana kusikojulikana, ndivyo itakavyokuwa Wilayani Ikungi
Mkoani Singida mara baada ya kutangazwa mashindano ya riadha
yanayojulikana kama Ikungi Half Marathon 2016.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya Jumamosi Septemba 3, 2016 katika Vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi.
Akizungumzia dhamira ya kuanzishwa kwa mashindano hayo Mkuu wa Wilaya
ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa itakuwa ni kuibua
vipaji kwa vijana na kuviendeleza, Kujenga umoja na mshikamano miongoni
mwa vijana na kuwaandaa vijana katika Wilaya hiyo kwa ajili ya
mashindano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Alisema kuwa
Mashindano ya mbio ndefu yenye umbali wa kilomita 21 yatahusisha vijana
wenye umri wa kuanzia miaka 17 hadi 30 waishio Wilayani Ikungi na
yatafanyika kila mwaka ili kuinua hamasa ya Mchezo wa riadha huku
yakiambatana na mbio fupi za mita 100, mita 200, mita 400 na mita 800.
Mashindano hayo yataanzia katika ngazi ya Vijiji Septemba 3, 2016,
ngazi ya Kata itakuwa ni Octoba Mosi, Ngazi ya Tarafa ni Octoba 15, 2016
na kwa ngazi ya Wilaya itakuwa ni Octoba 29, 2016.
Dc Mtaturu
alisema kuwa kuanzishwa kwa kuzinduliwa kwa mashindano hayo ni katika
kuhakikisha Wilaya ya Ikungi inaibua changamoto katika sekta ya michezo
nchini hivyo hiyo ni fursa muhimu kwa washiriki kujitokeza ili kuonyesha
uwezo wao katika kusakata riadha.
Mtaturu alisema kuwa mwaka
2017 panapo majaaliwa wamejipanga kufanya mashindano ya Ikungi Marathon
yatakayohusisha mbio ndefu za kilomita 42 ambapo jambo hili itakuwa ni
kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John
Pombe Magufuli.
Ameeleza kuwa mashindano hayo pia yamedhamiria
kuitambulisha Wilaya hiyo Kitaifa na Kimataifa kupitia shughuli
mbalimbali za kijamii ikiwemo michezo mbalimbali hususani mashindano ya
Riadha.
Aidha amewaomba vijana wote wenye umri uliofikia miaka 17
kujitokeza kwa wingi katika mashindano hayo ili kuimarisha afya zao na
kuachana na mawazo ovu yakiwemo yale ya kujihusisha na wizi na ujambazi,
Ngono zembe pamoja na ubakaji.
Kwa upande wake Afisa michezo
Wilayani Ikungi Abubakary Kisuda alisema kuwa mashindano ya ngazi ya
Vijiji yatafanyika kwa lengo la kupata vijana watakaoshindana ili
kushiriki mashindano ya ngazi ya Kata, ambapo mashindano ya Kata
yatafanyika kwa lengo la kupata vijana watakaoshindana ili kushiriki
mashindano ya ngazi ya Tarafa.
Kisuda alisema kuwa hili ni tukio
la awali kabisa kuanzishwa Wilayani humo tangu kuanzishwa kwa
Halmashauri ya Wilaya hiyo miaka mitatu iliyopita hivyo litaibua hisia
chanya na kuigwa na Taifa zima.