Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndg. Athumani J. Kihamia
amempuzisha kutekeleza majukumu yake Afisa Maendeleo ya Jamii
wa Jiji Bi. Mwantumu Dosi kwa tuhuma za kushindwa kutekeleza
majukumu yake hivyo kukiuka kanuni za Utumishi wa Umma za
mwaka 2003.
Mkurugenzi Kihamia ametoa taarifa hiyo Jana tarehe 27.08.2016
baada ya kukamilisha mbio za Mwenge wa Uhuru na kufanya
tathmini ya miradi iliyopitiwa na Mwenge na kugundulika kwa
dosari zilizojitokeza katika moja ya mradi ambao uko chini ya
Idara hii.
Mradi huo ni kikundi cha vijana wanaojishughulisha na Uselemara
pamoja na Uchomeleaji kinachojulikana kama Mbeshere Umoja
Group kilichopo Kata ya Olorieni kiligundulika kuwa na
wananchama waliovuka umri wa miaka 35 ambao hawastahili
kunufaika na Mikopo ya Vijana kwa mujibu wa Sera.
Mwenge wa Uhuru katika Jiji la Arusha ulikimbizwa tarehe
24.08.2016 na Kikundi hicho kilikua ni miongoni mwa miradi
iliyokua inapitiwa na Mwenge wa Uhuru ambapo wanachama wake
hawakizi vigezo. Wanachama hao walikua wameandaliwa kupewa
Hundi ya tsh Milioni tano kama ishara ya kuunga mkono jitihada
zao zakuboresha maisha. Mkimbiza Mbio za Mwenge Kitaifa Ndg.
George Jackson Mbijima alisitisha zoezi hilo baada ya kugundua
dosari za umri kwa baadhi ya wanachama.
Kupumzishwa kutekeleza majukumu ya Mkuu wa Idara hii
kunafuatana na masharti ya kukabidhi Ofisi kwa Mratibu wa Tasaf
Bi. Tajiel Mahega ambaye kwa sasa atakua Kaimu Mkuu wa Idara
hii mpaka pale uchunguzi utakapokamilika.
Nteghenjwa Hosseah
Afisa Habari, Halmashauri ya Jiji
Arusha.
27Agosti,2016