Ticker

6/recent/ticker-posts

DAWASCO KUTUMIA WIKI YA MAJI KUSIKILIZA KERO NA CHANGAMOTO ZA WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM.

                        Na Mwandishi wetu.

Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) limepanga kutumia maadhimisho ya 29 ya wiki ya maji inayoanza kesho kutoa elimu ,kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi kupitia Dawati maalumu katika vituo vyote 10 vya DAWASCO vilivyopo katika Jiji la Dar es salaam , Miji  ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.
Utaratibu huu umelenga kutoa mwanya kwa wananchi wanaopata huduma ya maji kutoka Dawasco ,kupata Elimu ya Huduma ya Maji  na kusikilizwa kero na malalamiko yao ili kujenga ukaribu zaidi kati ya DAWASCO na wananchi.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) Everlast Lyaro amesema madawati haya yatakuwa wazi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni kwa wiki nzima ya maadhimisho haya ya wiki ya Maji.
Amesema zoezi la kupokea kero na malalamiko kwa waanchi litafanyika hadi siku za Jumamosi na Jumapili ambapo Madawati yatakuwa wazi ili kutoa nafasi zaidi kwa wananchi wengi kuwasilisha changamoto zao na kupatiwa utatuzi.
Uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji utafanyika katika viwanja vya mnazi mmoja na mgeni rasmi anatazamiwa kuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda ambapo pamoja na mambo mengine Dawasco itapokea miradi ya Jumuiya za watumia maji katika maeneo mbalimbali.
Maadhimisho ya wiki ya Maji yameanza rasmi leo Machi 16 hadi Machi 22 mwaka huu yakibeba kauli mbiu ya “MAJISAFI NA MAJITAKA- PUNGUZA UCHAFUZI YATUMIKE KWA UFANISI
Wakati huo huo shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) linaendelea na zoezi maalum la ubadilishaji wa Mita za Maji  katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam pamoja na miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani Pwani.
Zoezi hilo lililoanza mapema October 2016, linalenga kuondoa mita zote za Maji ambazo ni chakavu, Mbovu  na zenye muda mrefu katika makazi ya watu, taasisi pamoja na viwanda ambalo linaenda sanjari  na ufungaji wa Mita mpya za Maji kwenye maeneo mbalimbali.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) Everlast Lyaro amesema tangu kuanza kwa zoezi hili tayari mita za Maji takribani 25,000 zimekwisha badilishwa na kwamba uondoaji wa mita Chakavu una lengo la kuongeza ufanisi katika usomaji wa Mita kwa usahihi, kupunguza kiasi cha Maji kinachopotea kutokana na uchakavu na kuakisi matumizi halisi ya Maji yanayotumiwa na mteja.

Mwisho.


Post a Comment

0 Comments