Hatimaye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemuachia kwa dhamana Mbunge wa
Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema baada ya kusota gerezani kwa
zaidi ya miezi minne.
Godbless Lema
Mahakama
hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja za pande zote mbili
zilizowasilishwa mahakamani hapo leo na kuamua kuzitupitilia mbali hoja
za upande wa serikali za kumnyima Lema dhamana.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache
kupita tangu mahakama rufaa kutupilia mbali rufaa ya jamhuri, huku
ikishangazwa na hatua ya Lema kukosa dhama hadi wakati huo.
Mbunge huyo ameachiwa kwa dhamana yenye
masharti ya wadhamini wawili wanaoaminika pamoja na kusaini bondi ya
shilingi milioni 1 ambapo nje ya mahakama Lema ametoa shukrani zake kwa
wote waliohusika na kubainisha kuwa serikali haikuwa na nia njema na
yeye, lakini yeye amesimama na Mungu.
"Ninamshukuru sana mwenyezi
Mungu, mke wangu, familia yangu, mawakili, viongozi wa chama na wananchi
wote waliokuwa na mimi. Na kwa namna ya pekee mke wangu, kama ningepata
nafasi ya kuoa tena, ningemuoa yeye. Pia mtoto wangu alifikia hatua
akasema anatamani kufanya kosa ili aje alale na mimi gerezani, na
akauliza ni kosa gani afanye ili aletwe gerezani" Amesema Lema
Baadhi ya viongozi wa CHADEMA waliokuwa wakifuatilia kesi mahakama kuu Arusha
Kwa upande wa wakili wake Peter Kibatala
amesema hatimaye kazi ya kwanza ya kuhakikisha Lema anapata dhamana
imekamilika na kwamba sasa wanajipanga kwa ajili ya kushughulika na kesi
ya msingi.
Kwa niaba ya CHADEMA, Mwenyekiti wake
Freeman Mbowe, amelaani nguvu iliyotumiwa na jeshi la polisi siku ya leo
ya kuwapiga, kuwakamata na kuwatawanya wafuasi wa chama hicho waliofika
mahakamani hapo kufuatilia kesi ya mbunge wao, huku akitangaza kuwa kwa
leo hakutakuwa na tukio lolote la kisiasa mpaka watakapotangaziwa tena.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia