Taasisi
ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na CUTS
International Geneva kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la
Maendeleo Sweden (SIDA), wamezindua Ripoti ambayo inaelezea namna bora
ya kuboresha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na kuiwezesha
Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama jinsi ulivyo Mpango wa Serikali
kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/17-2020/21.
Akizungumzia
ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dkt. Tausi Mbaga Kida
alisema, ripoti hiyo imeonyesha kuwa, kama viwanda vya ndani
vitaboreshwa vitawezesha kuwa na uwezo wa kuchakata mazao mengi ya
kilimo yanayozalishwa na wakulima zaidi ya asilimia 75 ya watanzania.
Pia
itasaidia kuongeza ajira, kuwahakikishia wakulima soko la uhakika wa
mazao yao, na serikali kujiongezea vyanzo vipya vya mapato kutokana na
bidhaa zitakazouzwa baada ya usindikaji na kwa kufanya hivyo, uchumi wa
wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara na wa Taifa kwa ujumla
utaongezeka.
“Utafiti
umeonyesha ili uweze kunufaika na kilimo lazima tuweze kuongeza thamani
katika mazao yetu na hilo tutaweza kulipata pale ambapo tutakuwa na
viwanda vyetu ambavyo vitaweza kuchakata mazao yetu katika ubora na
kuweza kuwafikia walaji sehemu mbalimbali. Kikubwa katika hilo ni jinsi
gani viwanda vya usindikaji, vikubwa na vidogo, vitaweza kuwa karibu na
wakulima,” alisema Dk. Kida.
Akisoma
hotuba ya uzinduzi wa Ripoti hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Viwanda na Biashara), Dr. Adelhem Meru,
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Masoko na Utafiti wa wizara hio, Bwana
Leo Lyayuka, alisema Serikali inafahamu kuwa katika safari ya kuelekea
katika nchi ya viwanda ni muhimu viwanda vyetu viwe na uwezo wa
kuchakata mazao ya kilimo ili kuyaongezea thamani.
Aidha
alitoa rai kwa Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO)
kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta ya usindikaji mazao
ya kilimo katika kubuni mashine zenye uwezo wa kuchakata mazao
mbalimbali na kuyauza ndani na nje ya nchi katika thamani kubwa zaidi.
Ndugu
Lyayuka alisema pia msingi mzima katika utafiti uliopo kwenye Ripoti
hio ni kuoanisha changamoto ambazo zipo katika mabadiliko ya tabia nchi
na jinsi gani zinaweza zikaathiri uzalishaji na usalama wa chakula,
biashara, na jitihada za kuendeleza viwanda vya usindikaji.
“Ni
muhimu sana kwa sera zetu za viwanda na kilimo kuoana ili kuchagiza
maendeleo haya ya sekta ya usindikaji, huku maswala mazima ya mabadiliko
ya tabia nchi yakitiliwa mkazo kuepukana na athari zinazoweza kuletwa
nazo.”
Kwa
upande wa mmoja wa watafiti, Ndugu Solomon Baregu alisema utafiti huo
ni muhimu kwa Tanzania na kama ukifanyiwa kazi kikamilifu unaweza
kuisaidia nchi kuingia katika uchumi wa viwanda.
“Utafiti
huu ni muhimu na umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatilia mkazo
sana suala la kujenga Tanzania ya viwanda. Sekta ya kilimo ni sekta mama
ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kuchochea ukuaji wa viwanda,” alisema Bwana Baregu.
Bwana Baregu aliongeza kuwa “Ni
muhimu sana Serikali kufikiria sasa kuja na sera mahususi itayoweza
kutambua ukuzaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo
(Agro-Industrial Development Policy) huku ikitilia maanani mabadiliko ya
tabia ya nchi na athari zake katika biashara, usalama wa chakula na
uchakataji mazao ya kilimo.”