JKCI KUANZA KUFANYA UPASUAJI WA KUPANDIKIZA MOYO

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatararajia kuanza upasuaji wa  kupandikiza moyo kwa wagonjwa wenye matatizo ya moyo nchini. 
Mkurugenzi wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya  Damu Dkt. Bashir Nyangasa ameyasema hayo leo Jijini, Dar es Salaam  alipokuwa akiongea na vyombo vya habari kuhusu malengo ya Taasisi hiyo. 
Tuko katika maandalizi ya kuandaa mapendekezo kwa ajili ya kupeleka  Bungeni ili Bunge lilidhie na kupitisha sheria itakayoruhusu mtu kuandika  wosia wa viungo vyake kutumika mara baada ya kufariki, ikiwemo moyo, figo  na viungo vingine,â€� alifafanua Dkt. Nyangasa. 
Aliendelea kwa kusema kuwa, umefika wakati kwa watanzania kujiwekea  utaratibu wa kuacha wosia wa kutumika kwa viungo vyao mara baada ya kufariki kwa ajili ya kuhifadhiwa katika benki za viungo ili viweze kutumika na watu ambao wanauhitaji. 
Aidha Dkt. Nyangasa amesema hospitali ya Apolo Bangalole ya India na  hospitali nyingine za kimataifa za magonjwa ya moyo kwa sasa zimehamia JKCI  kutokana na huduma pamoja na vifaa vinavyopatikana katika hospitali hizo  vinapatikana katika Taasisi hiyo. 
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Huduma za Tiba, Daktari Bingwa wa Wagonjwa  wa Moyo Dkt. Tulizo Shemu amesema kwa mwaka 2016 Taasisi imefanya uchunguzi  wa tiba kwa wagonjwa 973, kati ya wagonjwa hao 620 walipatiwa matibabu ya  moyo ya bila kufungua kifua kwa kupitia mishipa ya damu (Catheterization)  na wagonjwa 353 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua. 
Vilevile amesema kuwa kwa mwaka huu wa 2017 Taasisi hiyo imejipanga kufanya  upasuaji wa kupasua kifua kwa wagonjwa 700 na wagonjwa wengine 1000  watafanyiwa operesheni bila ya kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Catheterization.
Taasisi hiyo inategemea kuwa na kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa  kushirikiana na Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia  kuanzia Machi 10, 2017 ambapo wagonjwa 25 wakiwemo watoto 15 na watu wazima  10 watafanyiwa upasuaji. 
Wananchi wameombwa kujitokeza kuchangia damu kutokana na uhitaji wa damu  nyingi katika upasuaji huo.
Na Lilian Lundo –

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.