Ticker

6/recent/ticker-posts

KINANA LAZIMA UAMUZI WA RAIS SAMIA UUGWE MKONO


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg Abdulrahman Omar Kinana amesema uamuzi wa Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndg Samia Suluhu Hassan kufanya maridhiano ili kujenga umoja wa kitaifa ni mfano wa kuigwa na unapaswa kuungwa mkono.

Ndg Kinana amesema "Rais Samia Suluhu Hassan ameshakutana na baraza la vyama vya siasa pamoja na kituo cha demokrasia nchini na katika vikao na mikutano yote ameonesha utayari, nia na dhamira ya kujenga kuaminiana, kuvumiliana, kushirikiana na kuimarisha mazingira ya siasa nchini ili kwa pamoja tushirikiane kujenga nchi yetu."

Akiendelea kuwahutubia wanachama na viongozi wa CCM mkoa wa Arusha katika mkutano wa ndani kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Kinana amesisitiza "Nawasihi Wana-CCM wenzangu na vyama vingine vyote tuwe tayari kuunga mkono hatua hii nzuri ya maridhiano kwani kwenye umoja na ushirikiano ndiko kwenye maendeleo. Aidha katiba ya Nchi yetu inatambua nchi yetu ni nchi ya vyama vingi na lazima iendelee kubaki hivyo. Nchi yetu ikiwa na utulivu serikali inapata wakati mzuri wa kutekeleza wajibu wake kwa wananchi kikamilifu."

Wananchi waliojitokeza katika mkutano huo wameunga mkono kauli hiyo akiwemo Mbunge wa zamani wa jimbo la Longido na Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Arusha Mzee Lekule Laizer ambaye amesema "Ni vyema kila mtanzania mwenye nia njema akaunga mkono uamuzi huo wa kujenga maridhiano kwani una maslahi mapana na Nchi yetu."

Kinana alisema CCM ndio iliyopewa dhamana ya maendeleo ya Tanzania kupitia kuaminiwa na wananchi hivyo inayo jukumu la kuhakikisha umoja na mshikamano ili kazi za maendeleo zifanyike kwa utulivu.
 

Post a Comment

0 Comments