Teddy Kilanga, ARUSHA
Katika kuhakikisha bunifu zinaendelezwa nakuleta matokeo chanya katika jamii Baraza la jumuiya ya Afrika mashariki(EABC) kwa kushirikiana na Taasisi ya elimu ya juu ya chuo cha sayansi na Teknolojia Nelson Mandela wameandaa kongamano la kujadili namna ya kupata waatalamu wanaoendana na biashara katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.
Akizungumza jijini Arusha katika ufunguzi wa mkutano huo uliowakutanisha sekta binafsi na chuo cha Nelson Mandela ,Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella amesema lengo la majadiliano hayo ni kupata suluhisho la kibiashara ili kuleta maendeleo katika jamii.
"Ubunifu unaweza kusaidia kupata suluhisho mbalimbali za kibiashara katika kuleta maendeleo hivyo kwa mara ya kwanza tumeona EABC na chuo kikuu cha Nelson Mandela katika kuungana ili kuweza kutoa matokeo chanya ya biashara mbalimbali,"amesema Mongella.
Aidha amesema kuwa matokeo chanya hayo ni pamoja nakuzalisha rasilimali watu wenye uwezo wa kibiashara ili kuweza kujaza nafasi ya kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta ya biashara pamoja na uchumi wa viwanda.
"Pamoja na hayo ni vyema viwanda wakashirikiana na chuo cha Nelson Mandela ili kuweza kufahamu mahitaji ya masoko katika sekta zao ikiwa hata ushirika wa EABC na chuo cha Nelson Mandela umekuwa kwa vitendo zaidi,"amesema Mkuu huyo.
Naye makamu Mkuu wa chuo cha Nelson Mandela,Prof. Emmanuel Luoga amesema lengo ni kukuza bunifu zinazofanywa na wabunifu katika vyuo ili matokeo ya bunifu yanayopatikana waweze kuwasilisha katika sekta binafsi na kuzipeleka sokoni.
Prof.Luoga amesema vyuo vikuu ni sehemu ambayo inatoa maarifa kwa njia ya utafiti katika kuwafikia walengwa ambao ni wananchi hali ambayo itasaidia katika kuleta maendeleo.
Amesema wanafahamu kuwa serikali imeiachia sekta binafsi shughuli za viwanda na masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa yenyewe imebaki katika kutoa sera na njia ya utekelezaji wake hivyo kuna umuhimu wa matokeo yanayotolewa vyuo vikuu ni vyema yakaenda moja kwa moja kwenye sekta binafsi.
Vilevile Prof.Luoga amesema lengo ni kupunguza ombwe lililokuwepo la vijana hasa wanaofanya utafiti pamoja na sekta binafsi hivyo anaishukuru wizara ya elimu kwa kushughulikia masuala ya mitaala na kujikita katika vitendo zaidi.
Mwenyekiti wa EABC,John Bosco Kalisa amesema kupitia ushirikiano huo wataweza kuondoa upungufu wa wataalamu kwa kuongeza bunifu katika biashara kwani itasaidia kuleta tija katika jamii na kuinua uchumi wa viwanda.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia