Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)imetoa mafunzo kwa wachimbaji madini wadogo zaidi ya 80 jijini Arusha
Pia hivi karibuni ilifungia migodi sita ya madini ujenzi (Moramu )katika mkoa wa Arusha baada ya migodi hiyo kubainika kuwa ni hatarishi katika mazingira ya uchimbaji wa madini hayo na mingine kusabajisha vifo.
Akiongea wakati wa utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini meneja wa Nemc kanda ya Kaskazini ,Lewis Nzali alisema
Kuwa baraza hilo limeamua kufungia migodi hiyo ili kuepusha majanga ya vifo vya mara kwa mara katika migodi iliyobainika ni hatarishi.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu katika sekta ya madini,usalama mahala pa kazi na utunzaji wa mazingira ili kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea katika migodi hiyo kwa baadhi ya wachimbaji kufukiwa na kupoteza maisha kutokana na uelewa mdogo na dhana duni za uchimbaji.
"Kuanzia mwaka 2018 kumekuwepo na majanga yanayotokana na uchimbaji wa madini ujenzi ambapo mwaka 2018 watu wanne walifukiwa na kufa na gari moja kuharibiwa na wengine kujeruhiwa vibaya,mwaka 2021 watu kadhaa walifukiwa na kufa ikiwemo mifugo pia mwaka huu watu wamefukiwa na kufa"alisema.
Alisema hatua ya semina hiyo kwa wachimbaji ni maelekezo ya waziri wa nchi ,ofisi ya makamu wa rais muungano na Mazingira,dkt.Suleiman Jaffo ambaye alitembelea migodi hiyo na kutoa maelekezo ya kuwakutanisha wachimbaji wa madini ujenzi na kuwapaelimu ya ujimbaji salama.
Nzali alitoa rai kwa wachimbaji wa madini ujenzi kuhakikisha wanapata vyeti vya tathimini ya mazingira kutoka Nemc kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wa Moramu,Kokoto,mawe na Mchanga.
Naye afisa madini Mkazi Mkoani Arusha(RMO),Mhandisi Alphonce Bikulamchi,alisema semina hiyo ni muhimu sana katika sekta ya madini ili kuongeza makusanyo ya maduhuli ya serikali ikiwemo tozo na mirabaha na ada ya ukaguzi.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020 na 2021 sekta ya madini ujenzi mkoa wa Arusha ilichangia pato la taifa kiasi cha asilimia 21sawa na shilingi milioni 996.1
Alisema mwaka huu 2022 wanatarajia kuongeza makusanyo baada ya kujiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa semina kwa wachimbaji ili kupunguza vifo na ukusanyaji wa maduhuli kwa mfumo wa Kieletroniki.
Meneja wa Nemc kanda ya kaskazini Lewis Nzali akiongea na waandishi wa habari lengo la mafunzo hayo kwa wachimbaji madini ujenzi jana jiji Arusha.