HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA ARUSHA MOUNTMERU YAJA NA NJIA MPYA YA UTOAJI HUDUMA ZA KIAFYA KWA LENGO LA KUWA KARIBU NA WANANCHI




 Na Woinde Shizza, ARUSHA



Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 58 ya Mungano wa Tanganyaika na Zanzibar yanayofanyika kila mwaka Aprili 26,timu ya afya ya mkoa wa Arusha imetoa huduma za kibingwa za vipimo mbalimbali pamoja na tiba kwa wananchi kwa lengo la kutibu magonjwa yanayowasumbua watu.



Zoezi hilo linafanyika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha Mountmeru ambalo limekuwa likifanyika kila mara kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi.



Akizungumza baada ya kutembelea zoezi hilo,Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella amesema Uongozi wa hospitali hiyo imekuwa chachu katika kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi katika kutoa huduma za kibingwa bure kwa wananchi.



"Naishukuru timu ya afya ya mkoa wa Arusha na Utawala wa hospitali ya Mountmeru kwa kuendeleza zoezi hili ikiwa mwaka jana zoezi hili la kutoa huduma za afya,vipimo na dawa kwa baadhi ya magonjwa bure lilifanyika katika kipindi cha kusheherekea sherehe za uhuru wa nchi yetu,"alisema Mongella.



Aidha alisema kuwa katika zoezi hilo la hutoaji huduma za afya linaenda sambamba na utoaji wa dawa bure kwa baadhi ya magonjwa hivyo anawashukuru uongozi wa hospitali ya Mountmeru kwa kuwasaidia wananchi katika kupata matibabu.



Pia aliwashukuru wadau wengine katika juhudi zao za kufanikisha zoezi hilo kwani vitendo hivyo ni moja ya maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhitaji hospitali ziwe karibu na wananchi katika kutoa huduma za kiafya.



"Huu ni mfano mzuri sana badala ya kuwa karibu na wananchi badala ya kutegemea kila siku wananchi watoe fedha au bima kupata huduma lakini leo zinatolewa bure hivyo tuendelee kumshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuboresha miundombinu ya afya,"alisema Mongella.



Mongella alisema Serikali ya Rais Samia imeboresha miundombinu ya afya kwa kuanzia wataalamu wa afya kwani hapo awali madaktari bingwa walikuwa hawazidi 10 lakini sasa wapo takribani 25 hivyo hospitali hiyo inakwenda kwenye hadhi yake stahiki.



Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha Mountmeru,Dkt.Alex Ernest alisema kambi ya madaktari bingwa takribani 22 kutoka katika fani mbalimbali imetia kambi katika hospitali hiyo kwa lengo la kutoa hudumia wananchi wa mkoa wa Arusha pamoja na maeneo ya jirani.



Dkt.Ernest Alisema huduma hizo za kiafya hutolewa bure kuanzi kumuona daktari pamoja na dawa hivyo wanawashukuru wadau walichangia dawa zenye thamani zaidi ya sh.milioni 30 ambazo zinatolewa wananchi walibainika na magonjwa mbalimbali kama sehemu ya kuadhimisha siku hiyo.



"Lengo la serikali yetu ni kutaka kuona wananchi wake wanakuwa na afya boro iliyohimarika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hivyo mwitikio ni mkubwa kwa upande wa wananchi ikiwa hadi sasa tumewahudumia zaidi ya wagonjwa 2400 na kulingana na uhitaji mkubwa kwa wananchi na sisi tutaendelea kutoa huduma sehemu mbalimbali katika maeneo yao ili kuweza kuwafikia zaidi,"alisema.


Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post