Ticker

6/recent/ticker-posts

KUKAMILIKA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA POSTA AFRIKA KUTAWANUFASHA WANANCHI

 Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka hiyo mbele ya jengo la sasa la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya PAPU. Bodi hiyo imeeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi. PICHA: TCRA

**************

Na Mwandishi Wetu

Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Posta barani Afrika (PAPU) unaoendelea jijini Arusha kumetajwa kuwa kutawanufaisha wananchi na wadau mbalimbali katika jiji hilo kwa kuwa matumizi ya jengo hilo yanatarajiwa kuwa zaidi ya ofisi za Umoja huo.

Akizungumza jijini Arusha muda mfupi baada ya kuongoza ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Menejimenti ya Mamlaka hiyo kukagua Maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa Kumi na Saba litakalogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 30 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jones Kilimbe amefafanua kuwa jengo hilo litatumiwa pia kwa shughuli mtambuka za kijamii na kiuchumi kama vile kuwemo eneo la soko kubwa (Mall), eneo la watalii kutazama vivutio na ofisi nyingine zitakazotumiwa na wadau wengine mbali na Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika.

“Tuko sambamba na Maendeleo ya jengo hili, ili tuje tuone matokeo chanya ambayo tunayategemea yatakuwepo mbele ya safari” aliongeza Kilimbe na kufafanua kuwa ujenzi na kukamilika kwa jengo hilo itakuwa ni sehemu ya kutimiza ndoto za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambae alipendekeza kwa uliokuwa Umoja wa Afrika wakati huo kujengwa kwa makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika nchini.

“Ni taasisi chache sana ambazo zinafanyiwa vitu kama hivi ambazo zinajengewa jengo kubwa kama hili na la hadhi; jengo hili lina umuhimu mkubwa na sasa hivi tunadhihirisha kuwa Tanzania tunastahili kuwa Makao Makuu ya PAPU, kulikuwa na watu walifikiria huenda wangeweza hata kubadilisha hiyo sifa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya PAPU kwa kuwa hatujawapa jengo la kutosha, kwa hiyo kwa ujenzi huu manufaa ni makubwa” alibainisha Kilimbe.

Akizungumzia uwezekano wa Taasisi nyingine za TEHAMA kikanda na Kimataifa kufikiria kuweka Ofisi zao za Makao Makuu au ya kanda, amebainisha kuwa Suala hilo litawezekana kwa kuwa kukamilika kwa jengo la PAPU kutawavutia wadau kuifikiria Tanzania ili kuweka ofisi zao kwa kadri itakavyowafaa.

Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA wakiwa sambamba na Menejimenti ya Mamlaka hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari Jumatano ya Aprili 27 umetembelea mradi wa ujenzi wa jengo hilo ili kujionea Maendeleo ya ujenzi, ambao kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ujenzi unaendelea vizuri kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari ameeleza kuwa Menejimenti imeandaa ziara hiyo ili kuiwezesha Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA kujiridhisha na ujenzi ikizingatiwa kuwa ndiyo Msimamizi wa Mamlaka ya Mawasiliano na ujenzi wa Ofisi hizo unajengwa kwa ushirikiano wa TCRA na PAPU.

Aidha amebainisha kuwa jengo hilo mbali na Ofisi za PAPU litakuwa na ofisi za Shirika la Posta Tanzania, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini ya TCRA lengo likiwa kusogeza huduma mahali pamoja ili kumwondolea usumbufu Mwananchi anapohitaji huduma za mawasiliano. Kuhusu zoezi la anwani za makazi Bakari alisisitiza kuwa zoezi hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa litaondoa kabisa adha ya upatikanaji huduma za Posta kwa wananchi mara litakapokamilika.

“Tunaandaa wananchi kupokea vifurushi kwa urahisi; na Posta sasa imeendelea na imeenda dijitali na sasa posta itarahisisha biashara na bila shaka Posta ni hatua muhimu na jumuishi katika ukuzaji wa Uchumi wa Kidijitali” alibainisha Dkt. Bakari na kuongeza.

Zaidi ya shilingi bilioni 38 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la kisasa lenye jumla ya ghorofa 17 ambalo linajengwa kwa ubia kati ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA)

Post a Comment

0 Comments