Mfanyabiashara Maarufu wa Madini ya Tanzanite Jijini Arusha,Pendael Mollel na wenzake watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mlinzi.
Kukamatwa kwa Mfanyabiashara huyo na wenzake watatu kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,Justin Masejo na kueleza kuwa mtuhumiwa alikamatwa mjini Moshi alikokimbilia na kujificha baada ya tukio hilo.
Masejo alisema kuwa watuhumiwa wote wako rumande katika kituo kikuu cha Polisi Arusha kwa ajili ya mahojiano na kuna baadhi ya watuhumiwa wengine wanasakwa na polisi ili kuunganishwa katika tukio hilo.
Alisema kwa sasa siwezi kusema chochote zaidi ya kujua kuwa watuhumiwa wako rumande ila baada ya siku moja ama mbili wahusika wakikamilisha kutoa maelezo ataweza kutoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya tukio hilo.
‘’Ninachoweza kusema kwa sasa ni kukiri kuwa mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite Pendael Mollel tumemkamata Moshi kwa tuhuma za mauaji na wenzake watatu wamekamatwa Arusha na wako kwa ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha{RCO}’’ alisema Kamanda Masejo
Habari kutoka vyanzo vya eneo la tukio Burka karibu na uwanja wa ndege wa Arusha zilidai kuwa tukio hilo la mauaji lilitokea aprill 18 mwaka huu majira ya saa 1.45 usiku ambapo Mollel akiwa na wapambe wake walikwenda kumchukua marehemu aliyetambuliwa kwa jina la Stephen Jimmy Kivuyo{43} katika nyumba anayokuwa akilinda inayomilikiwa na Mtanzania mwenye asili ya Kisomali aliyetambuliwa kwa jina la Mahamudu Mohamed.
Vyanzo vya habari vilidai kuwa kabla ya kutekwa kwa marehemu na Mollel na wapambe wake jioni ya siku hiyo tajiri huyo wa Madini ya Tanzanite aliwasiliana na Mohamed mwajiri wa mlinzi huyo na kudai kuwa mlinzi wake ameiba Pampu ya kusukuma maji yenye thamani ya shilingi 180,000 .
Habari zilidai kuwa mwajiri wa marehemu aliwasiliana na mafundi walioko eneo la nyumba yake na kueleza malalamiko ya jirani lakini mafundi walimhakikishia kuwa mlinzi siku hiyo ya tukio hakuweza kutoka siku hiyo kwani walikuwa wote lakini alipoelezwa Mollel hakukubaliana na kauli hiyo na kudai kuwa polisi wacha wafanya kazi yao.
Vyanzo vilidai kuwa Mollel akiwa na wapambe na watu wengine walimteka marehemu na kumwingiza katika nyumba ya tajiri huyo na kuanza kumpa kichapo na baada ya muda mfupi mtuhumiwa huyo qpq alipoteza maisha.
Habari zilidai kuwa baada ya kichapo hicho cha Mollel kwa kushirikiana na wapambe wake tajiri wa Madini ya Tanzanite aliamuru marehemu kupelekwa polisi kwa Mrombo na kuwaeleza polisi kuwa wananchi wenye hasira wamemuua hatua ambayo polisi waligoma kupokea maiti na kuwaelekeza kupeleka chumba cha maiti katika hospital ya Muriet ambapo maiti iko hadi sasa ikisubiri kufanyiwa uchunguzi.
Naye Mjomba wa Marehemu,Ernest Julius alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani alisema kuwa kwa sasa hawawezi kusema chochote juu ya kifo cha ndugu yake ila alidai kuliachia jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kwani marehemu hana tabia ya udokozi kwani amefanya kazi ya ulinzi kwa Tajiri Mahamud Mohamed kwa muda mrefu bila ya matatizo.
Julius alisema mwili wa marehemu uko katika chumba cha maiti katika hospital ya Muriet na wameshindwa kuuchukua kwa kuwa polisi bado hawajaufanyia uchunguzi wa mwisho na wameambiwa uchunguzi ukikamilika wataruhusiwa kuuchukua na ndio siku ya maziko itajulikana.
Naye Mwajiri wa Marehemu,Mahamudu Mahamed alisema kuwa marehemu amefanya naye kazi kwa muda wa zaidi ya miaka miwili na hakuwa na tabia ya wizi kwani alikuwa akimwachia pesa nyingi kwa ajili ya kuwalipa mafundi wa ujenzi wa nyumba yeke iliyopo Burka.
Mohamed alisema alipigiwa simu na Mfanyabiashara Mollel juu ya kilio chake cha kuibiwa Pampu ya kusukuma maji na kumtuhumu marehamu lakini alimkatalia na kusema kuwa afanye uchunguzi vizuri anaweza kumjua mwizi wake hatua ambayo ilipingwa na tajiri huyo wa madini ya Tanzanite.
Alisema aprill 17 mwaka huu Molle alidai kuibiwa hiyo Pampu na Aprill 19 mwaka huu aliingia katika nyumba yake na kumchukua mlinzi wake kwa madai kuwa walinzi wa mfanyabiashara huyo ndio waliomwambia kuwa ndio aliyeingia na kuichukua pampu hiyo na kuamua kuondoka naye.
Mahamed alisema amewachukua mafundi wake,walinzi wengine wameshakwenda kutoa maelezo juu ya tukio hilo katika kituo kikuu cha polisi Arusha mengine jeshi la polisi litajua la kufanya ila kifo cha mlinzi wake kimemsikitisha sana kwani hakuwa na tabia hiyo.