BREAKING NEWS

Thursday, April 21, 2022

HIVI NDIVYO NAIBU WAZIRI WA MADINI ALIVYOFAFANUA KUHUSU RUBY YA DUBAI

 

 


 
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa ufafanuzi kuhusu Jiwe la Madini  ya Ruby  lenye uzito wa kilo 2.8 lililooneka Dubai ambalo linasadikika kutoka Tanzania na kueleza  kuwa, wizara inaendelea  kufuatilia ukweli wa taarifa zake  na endapo itapata nyaraka kuhusiana na jiwe hilo kama limetoka Tanzania, Taratibu na Sheria za Tanzania zitatumika katika kupata haki ya Tanzania.


Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mkinga Dunstan Kitandula ambaye alitaka kujua namna ambavyo Tanzania itanufaika na jiwe hilo. Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa, jiwe hilo linalosemekana kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 120 ambazo ni sawa na zaidi ya  shilingi bilioni 240 za kitanzania, taarifa zake zilionekana zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wizara ilipata taarifa zake tarehe 13 Aprili, 2022.

Ameongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, wizara  ilichukua hatua za haraka ili kujua kama habari hizo ni za kweli kwa  kuanza kufanya ufuatiliaji kwa kuangalia taarifa za usafirishaji wa madini ya aina hiyo kwenye kanzidata zake na kubaini kutokuwepo kwa taarifa zinazofanana za jiwe hilo kwa uzito na thamani.

Akizungumzia mmliki halali  wa jiwe hilo, amesema inasemekana huenda yupo nchini Marekani katika Jimbo la California na  katika ufuatiliaji wa kupata chanzo halisi na asili ya jiwe hilo, nchi tatu  (3) zinahusishwa ikiwemo Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu-Dubai na Tanzania.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa wizara inawahakikishia watanzania kwamba itaendelea kusimama imara katika kudhibiti na kulinda rasilimali za watanzania kwa manufaa ya nchi hiyo.

Inaelezwa kuwa, jiwe hilo linatarajiwa kuwekwa kwenye mnada wa mauzo ya madini baada ya mfungo wa Ramadhan kuisha na baada ya kutembezwa ili kuoneshwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Awali, Dkt. Kiruswa akijibu swali la Mbunge wa Rolya Jafari Wambula ambaye alitaka kujua ni lini uchimbaji wa madini utaanza katika eneo la Utebi ambapo Dkt. Kiruswa amesema, eneo hilo litaanza kuchimbwa mara baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kukamilisha utafitka ambao umeanza kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia, Dkt. Kiruswa amesema upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji ya madini kwa wachimbaji wadogo utafuata mara baada ya utafiti kukamilika ambapo pia, amesema wizara yake inaendelea kujenga vituo vya ununuzi na uuzaji wa madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo Liwale.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates