Wizara ya Afya kuanza kukagua ubora katika vituo vya kuyolea huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa Jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi katika mkutano wa viongozi wa vyama vya kitaaluma vya Afya uliofanyika jijini Dar es salaam.
Prof. Makubi amesema kuelekea uboreshaji wa huduma za afya Serikali kupitia wizara ya afya itaanza kufanya ukaguzi katika hospitali ili kuona kama zinatoa huduma bora kwa wananchi.
"Kuanzia wiki ijayo tutaanza na hospitali ya Taifa Muhimbili tunataka kukagua ubora wa huduma, kwa kushirikiana na menejimenti na vyama vya kitaaluma ili tuweze kuboresha maeneo ambayo yanalalamikiwa na wananchi." Amesema.
Prof. Makubi amesema tunataka watumishi wa sekta ya afya kuboresha utoaji wa huduma za afya kama ilivyo ajenda ya kwanza kwenye sekta ya afya mwaka huu
"Tunachotaka kuona sasa hivi ni ubora gani mwananchi amepata anapoenda kwenye kituo kwa kupokelewa kwa lugha nzuri na wahudumu, kusikilizwa na daktari kwa lugha nzuri, kupata vipimo kwa usahihi, kupata dawa ambazo ameandikiwa na daktari".
Vile vile Prof. Makubi amewataka watumishi wa sekta ya afya kuwahudumia wagonjwa kwa muda mfupi pindi wanapohitaji huduma na kuwahudumia kwa ubora wa hali ya juu
"Tuachane na tabia ya mwananchi anaenda kwenye kituo anakaa kuanzia saa mbili mpaka saa nane bila kupata huduma, tuanze kupunguza muda wa kuwahudumia wananchi pia tuwahudumie kwa ubora"
Aidha,Prof. Makubi amevitaka vyuo vya afya nchini kutoa elimu bora ili kuweza kupata wataalamu wenye viwango vya kuweza kulinda maisha ya wananchi.
"Tumegundua kuna tatizo katika ufundishaji wa wanafunzi kwa baadhi ya vyuo vya afya, tutashirikiana na wizara ya elimu kurekebisha changamoto hizo ilikuweza kupata wataalamu wenye viwango." Amesema
Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt . Aifello Sichalwe ametoa wito kwa wasimamiaji wa huduma kuhakikisha wanafuata ubora wa huduma kwa wananchi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuzuilika ikiwemo vifo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Sichalwe ametoa wito kwa Wanataaluma kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa (survaillence) ili kutambua mapema magonjwa, ikiwemo magonjwa ya mlipuko na kuweka mikakati mizuri ya namna bora ya kupambana dhidi ya magonjwa hayo kwa kushirikiana na Serikali.
Kwa upande wake msajili wa Baraza la famasia Bi. Elizabeth Shekalaghe ametoa wito kwa wanataaluma wa afya wote nchini kuhakikisha wanazingatia sheria kanuni na miongozo katika utendaji kazi wao.
" Faini kwa wanataaluma wanao fanya makosa zipo, kwa hiyo nitoe wito kwa wanataaluma wote nchini kufuata sheria kanuni na miongozo wakati wa kutoa huduma."
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia